Serikali imepanga kuendesha zoezi maalumu la usajili na utoaji wa utambulisho na vitambulisho vya Taifa kwa Watumishi wa Umma nchi nzima litakalodumu kwa muda wa wiki mbili kuanzia Oktoba 3, 2016.
Watumishi watakaosajiliwa ni waliopo katika Wizara, Idara za serikali zinazojitegemea, Tawala za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Wakala za Serikali na Taaaisi, Mashirika ya Umma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Angellah Kairuki wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam amesema lengo la zoezi hilo la usajiri ni kuondoa vyanzo vya watumishi hewa vinavyotokana na utambulisho danganyifu.
“Serikali inaendelea na zoezi la kuandaa utaratibu mmoja wa kukusanya, kutunza, kutumia na kuhifadhi taarifa muhimu ili kuwa na chanzo kimoja sahihi. Hatua hii itapunguza gharama za uendeshaji, kuongeza tija, ufanisi na uwazi serikalini, ” amesema na kuongeza.
“Lengo ni kuunganisha mifumo ya utambuzi wa watu na mifumo mbalimbali ikiwemo usimamizi wa rasilimali watu na mishahara katika utumishi wa umma, pia utasaidia kuondoa vyanzo vya watumishi hewa vinavyotokana na utambulisho danganyifu.”
Kairuki amesema usajili huo utaambata na uhakiki wa vyeti vya elimu, vya kuzaliwa, hati ya kusafiria, kitambulisho cha kupigia kura na karatasi za malipo ya mishahara ya watumishi hao.
Aidha, amesema watumishi watakaokaidi agizo hilo watachukuliwa hatua za kisheria kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa umma.
“Data zilizopo ni chafu, wakati mwingine ukifuatilia taarifa ya mtumishi unakuta taarifa ya cheti cha kuzaliwa au elimu hakuna. Usajili huu utavumbua mengi na wale wasio na sifa watajifukuzisha kazi wenyewe, ” amesema.
Kairuki amezitaka ofisi na taasisi zote za serikali kuandaa ratiba itakayowezesha watumishi kufanya usajili pamoja na kutoa ushirikiano wa kutosha ili kufanikisha zoezi hilo.
Na Regina Mkonde