Baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba kukituhumu chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuwa kinaivuruga chama chake. Chadema imekanusha madai hayo na kudai kuwa Lipumba ndiye msaliti wa harakati za kutetea masilahi ya demokrasia nchini na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Mwenyekiti wa Chadema Taifa Freeman Mbowe leo amesema kuwa chama hicho sambamba na viongozi pamoja na wafuasi wake hawamtambui Lipumba kuwa ni Mwenyekiti wa CUF na kwamba chama hicho hakitatoa ushirikiano kwake na hata kwa wafuasi wake.
“Kamati maalumu ya kamati kuu imepokea taarifa ya mgogoro unaondelea ndani ya CUF unaomhusisha aliyekuwa mwenyekiti Taifa wa chama hicho Profesa Ibrahim Lipumba, pia kamati inatambua kuwa mgogoro huu unachochewa na utawala wa kiimla wa Rais Magufuli kwa kumtumia Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi, ” amesema.
“Kamati inavielekeza vyombo vyote vya chama chetu, viongozi wa ngazi, wanachama na wafuasi wa chama chetu na wapenda demokrasia wote nchini kumuangalia Lipumba kama msaliti wa harakati za kudai haki nchini na kutokumpa yeye na wafuasi wake ushirikiano wa aina yoyote ,” amesema.
Katika hatua nyingine viongozi wa vyama vinavyounda umoja huo, wameandaa mkutano utakao fanyika kesho jijini Dar es Salaam wenye lengo la kumjadili Lipumba.
Mgogoro wa CUF unaondelea sasa huenda ukapelekea chama hicho kujiondoa katika UKAWA na au kutotekeleza baadhi ya makubaliano ya umoja huo.
Kwa sababu, leo Lipumba ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho, ametamka hadharani kuwa CUF iko tayari kusimamisha mgombea wake katika uchaguzi mkuu ujao na kudai kuwa umoja huo hauna mamlaka kikatiba ya kusimamisha mgombea kwa niaba ya vyama vyote vinavyounda umoja huo.
Moja ya makubaliano ya Ukawa ni kuwa unasimamisha mgombea mmoja wa urais kutoka chama kimoja, atakayeungwa mkono na vyama vinavyounda umoja huo, jambo ambalo linaonekana kutoungwa mkono na Lipumba aliyekiri kuwa chama chake hapo baadae kitasimamisha mgombea wake.
Licha ya kauli hiyo ya Lipumba kudhihirisha kuwa haungi mkono UKAWA, pia ameutuhumu umoja huo kuwa umepotea kisiasa na kwamba vyama vinavyounda umoja huo vimeshindwa tekeleza adhma yake ya kupambana na rushwa, ufisadi na kuitetea rasimu ya katiba ya jaji Joseph Warioba baada ya kumpokea Edward Lowassa aliyemtuhumu kuwa aliipinga rasimu hiyo.
Lipumba alisema kuwa “Ukawa imepotea kisiasa baada ya kumpokea Lowassa, imeacha kupambana na rushwa, ufisadi na badala yake Rais Magufuli ndiyo anatekeleza na kupambana na vita hiyo.”
Ameongeza kuwa “Lengo la Ukawa ni kuitetea rasimu ya Warioba, awali lowassa hakuitetea na hakuiunga mkono. Wananchi waelewe kuwa Ukawa si chama cha siasa na imesahau majukumu yake ya kupigania rasimu ya katiba ya warioba.”
Endapo Lipumba ataendelea na wadhifa wake huo na kuendelea na misimamo yake ya kutokubali umoja huo kumuunga mkono Lowassa, ikiwa Ukawa itamchagua Lowassa kugombea urais 2020, anaweza akaumegua umoja huo kutokana na misimamo yake.