WINGA Shiza Ramadhani ‘Kichuya’, amesema yupo tayari kuondoka Simba na kwenda kucheza soka la kulipwa iwapo Klabu ya Chippa United ya Afrika Kusini itamhitaji.
Klabu ya Chippa United imevutiwa na Kichuya baada ya kuonyesha uwezo wa hali ya juu wa kucheza soka Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ambaye kwa sasa anaongoza kwa kufunga mabao saba.
Akizungumza na BINGWA jana Kichuya alisema malengo ni kutaka kucheza soka ya kulipwa nchi ya Tanzania kama ilivyo kwa Mbwana Samatta anayekipiga Genk ya Ubelgiji na Thomas Ulimwengu, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Kichuya alisema hawezi kuikataa ofa itakayokuja mbele yake lakini wanaomhitaji ni lazima wazungumza na wakala wake na Simba kwani bado ana mkataba na klabu hiyo.
“Nipo tayari kwenda kucheza soka nchi yoyote ili niweze kutimiza malengo yangu, lakini inafahamike kuwa mimi si mchezaji huru nina mkataba na Simba,” alisema Kichuya.
Alisema licha ya kwamba ana mkataba na Simba, lakini kwa kushirikiana na meneja wake ni lazima waangalie aina ya ofa inayokuja, kwani nyingine zimekaa kiujanja ujanja.
“Unajua si kila ofa unaitolea macho na kuikubali kwani mjini hapa ujanja mwingi, kikubwa ni kukaa mezani baina ya meneja wangu, uongozi wa Simba na hao watakaonihitaji kuona kuna masilahi gani kwangu.”
Kichuya alijiunga na Simba msimu huu wa ligi kuu kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Mtibwa Sugar aliyoitumikia kwa takribani misimu mitatu
0 comments :
Post a Comment