Mapigano
yamerudi upya mjini Aleppo masaa machache baada ya kumalizika muda wa
usitishaji mapigano uliotangazwa na Urusi, huku Umoja wa Mataifa ukisema
kuwa serikali ya Syria imetumia silaha za kemikali.
Afisa
mmoja wa Shirika la Msalaba Mwekundu alisema hadi sasa hakuna raia
aliyeweza kuondolewa ndani ya siku tatu za kusitishwa kwa mapigano,
ambako Urusi ilisema kulikusudiwa kuruhusu raia na majeruhi kuondoka
kwenye eneo la mashariki mwa mji wa Aleppo, ambalo linashikiliwa na
waasi.
"Kuwaondoa
watu hakukuwezekana kwa sababu ya hali mbaya ya usalama kwenye mji
huo," alisema msemaji wa shirika hilo nchini Syria, Ingy Sedky,
akiongeza kuwa timu ya maafisa wa shirika lake walishindwa kuingia eneo
la mashariki mwa Aleppo, ambalo limezingirwa na majeshi ya serikali
tangu mwezi Julai, kutokana na makombora yanayorushwa na pia kuwapo kwa
wadunguaji kwenye majengo.
Shirika
la Uangalizi wa Haki za Binaadamu la Syria lilisema kuwa mwisho wa
usitishaji huo wa mapigano ulitandwa na mapigano katika maeneo ya
Amiriyeh, Salah al-Din na Sheikh Said.
Kwa
mujibu wa shirika hilo, ndege za kivita zilipaa kwenye eneo la kati la
Aleppo na kufanya mashambulizi kwenye eneo moja kwenye viunga vya mji
huo, ambako hivi karibuni waasi walikuwa wamevizidi nguvu vikosi vya
serikali.
Jeshi la
Urusi lilikuwa limetangaza usitishaji mapigano wa masaa 11 siku ya
Alhamis ili kuwaruhusu raia, waasi na majeruhi kuondoka kwenye eneo
hilo, wakiwaahidi usalama wao. Baada ya hapo, iliongeza muda wa
usitishaji huo wa mapigano kwa siku mbili zaidi. Hata hivyo, waasi
walisema wasingeliondoka kwenye mji huo.
Upinzani
nchini Syria ulisema hakukuwa na hakikisho endapo watakaoondolewa
wasingelikamatwa na vikosi vya serikali na wala nafasi ya kuwapa misaada
ya kibinaadamu wale wanaobakia kwenye eneo hilo lililozingirwa.
Sedky
alisema siku ya Ijumaa kwamba wafanyakazi wa Shirika la Msalaba Mwekundu
walikuwa tayari kuwaondoa watu kutoka eneo hilo, lakini hawakuwa
wamepokea hakikisho muhimu la usalama wao.
Kati ya
raia 250,000 na 300,000 wanakadiriwa kuwa wamenaswa mashariki mwa
Aleppo, wakiwa hawana chakula wala madawa ya kutosha, huku hospitali
zinazowatibu majeruhi nazo zikiwa zinashambuliwa kwa mabomu kutokea
angani.
Umoja wa Mataifa wasema Syria yatumia silaha za sumu
Mtoto aliyesambuliwa kwa silaha za sumu kaika mji wa Idlib, Syria.
Wakati
huo huo, waangalizi wa Umoja wa Mataifa wamehitimisha kwamba utawala wa
Syria ulitumia gesi ya klorini kwenye mashambulizi yake ya tatu ya
kemikali mwaka jana.
Ripoti
iliyovuja kutoka Shirika la Kuzuia Silaha za Kemikali (OPCW) hapo
Jumamosi (22 Oktoba) inasema kuwa helikopta za serikali ya Syria
ziliangusha mabomu ya matangi yakiwa na gesi ya klorini kwenye eneo la
kaskazini magharibi mwa mji wa Idlib mwezi Machi 2015.
"Tunaulaani
vikali utawala wa Bashar al-Assad kwa kuvunja miiko ya kilimwengu
katika matumizi ya silaha za kemikali na ukiukaji wa Syria kwa majukumu
yake chini ya Mkataba wa Kuzuia Silaha za Kemikali ambao ilisaini mwaka
2013," alisema msemaji wa Ikulu ya Marekani, Ned Price.
Marekani
imezitolea wito Urusi na Iran kuungana na jitihada za kimataifa za
kuiwajibisha serikali ya Syria kutokana na matumizi yake ya silaha za
kemikali na kuacha mara moja kuusaidia utawala wa Assad.
"Ripoti
hiyo ya OPCW inathibitisha tukio la tatu la matumizi ya klorini
yaliyofanywa na utawala na kuweka wazi ushahidi kwamba serikali ya Assad
inatumia kemikali za sumu kwa makusudi, ikivunja sheria za kimataifa,"
alisema Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, Samantha Power.
Hayo
yanatokea wakati Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa
likiamua kuanzisha uchunguzi wa uhalifu wa kivita dhidi ya watu wa
Aleppo, hatua ambayo inazipa shinikizo serikali za Syria na mshirika
wake Urusi, ambazo zimekuwa zikilitwanga kwa mabomu eneo linaloshikiliwa
na waasi mashariki mwa Aleppo.
Chanzo:DW


0 comments :
Post a Comment