Wakati Kampeni za kinyang’anyiro cha kuingia Ikulu ya White House zikiendelea kupamba moto nchini Marekani huku kila mgombea akijinadi kwa Wamarekani kwa kumkosoa mpinzani wake.
Donald Trump amevishutumu vyombo vya habari nchini humo kwa madai kuwa vimeripoti habari za uwongo dhidi yake kwamba aliwadhalilisha wanawake kingono. Tuhuma hizo dhidi ya Trump zilitolewa wakati mke wa rais Barack Obama, Michelle Obama akihutubia wananchi katika mkutano wa kampeni ya kumpigia debe mgombea wa chama cha Democratic Hillary Clinton mjini New Hampshire.
Katika mkutano huo Michelle Obama alimshambulia kwa ujumbe mkali mgombea huyo wa Republican kwa kudai kuwa, Trump anastahili kukomeshwa tabia yake ya kudhalilisha wanawake huku akisisitiza kuwa hajatoa shutuma hizo kwa sababu Trump yupo chama pinzani.
“Haijalishi uko chama gani, Democratic, Republican, au asiye na chama. Hakuna mwanamke anayestahili kufanyiwa hivi, aina hii ya dhuluma. Nafahamu hii ni kampeni, lakini hili halihusu siasa, ni kuhusu maadili ya ubinaadamu, ni kuhusu kizuri na kibaya na hatuwezi kuendelea kuvumilia hilo au kuwaweka watoto wetu katika hali hii sio tu dakika moja bali miaka minne ijayo. Ni wakati wa sisi sote kusimama na kusema inatosha sasa”. alisema Bi Obama.
Lakini Trump mwenye umri wa miaka 70 alisimama kidete, akiwakemea wakosoaji wake kuwa ni “waongo wakubwa” na kumshtumu Bi Clinton kwa kula njama na vyombo vya habari ili kuhujumu kampeni yake.
Hata hivyo, karibu wanawake sita wametuhumu Trump kwa kujaribu kuwapapasa na kuwabusu kwa lazima katika matukio yaliyoripotiwa na vyombo vya habari vya New York Times, NBC, People Magazine.