Mabingwa watetezi wa VPL, Ligi Kuu Vodacom Tanzania Bara, Yanga,  leo Oktoba 26 imeendeleza wimbi la kutoa dozi kwa timu inayokutana nayo ambapo  wameitandika bila huruma timu ya Maafande Ruvu JKT bao 4-0, mchezo uliomalizika jioni hii.
Mchezo huo wa kiporo uliochezwa katika uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam,  Wanajangwani hao wameweza kushuka kwa mara ya kwanza bila ya Kocha wao Mholanzi Hans van de Pluijm ambae amejiuzulu baada ya Klabu hiyo kumwingiza ‘kinyemela’ Kocha Mpya kuchukua nafasi yake.
VPL hivi sasa inaongozwa na Simba wenye Pointi 29 kwa Mechi 11 na Yanga wapo Nafasi ya Pili wakiwa na Pointi 21 kwa Mechi 10.
Awali Yanga, waliibamiza Kagera Sugar 6-2 katika Mechi yao iliyopita, hivyo kwa ushindi wa leo wa bao 4 ni kielelezo tosha cha kuendeleza dozi.
Wapinzani wao wa jadi  Wekundu wa Msimbazi wao wanashuka  Jumamosi ya  Oktoba 29 wakicheza Ugenini huko Shinyanga na Mwadui FC.
Kipigo hicho cha bao 4, kinaendelea kuiweka Ruvu JKT   kizani kwani hadi sasa imeshinda Mechi 1 tu, Sare 6 na Kufungwa 5 hali iliyowaacha Nafasi ya Pili toka Mkiani hadi sasa.