Maonyesho Ya Uhuru Kuhamia Mkoani Dodoma

Sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Tanzania Bara zitakuwa zikifanyika mjini Dodoma kuanzia mwaka 2017 badala ya Jijini Dar es Salaam kama ilivyozoeleka.
 
Uamuzi huo umetangazwa leo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya Ulinzi na Usalama Dkt. John Magufuli, wakati akitoa salamu zake za maadhimisho ya miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania Bara, kwenye sherehe zilizofanyika leo katika uwanja wa Uhuru dar es Salaam.

Katika salamu hizo, Rais Magufuli ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi, ameeleza sababu za kufuta sherehe hizo mwaka jana na kuruhusu mwaka huu zifanyike ambapo amesema sababu moja wapo iliyomfanya afute sherehe hizo mwaka jana ni kubana matumizi.

"Mwaka jana nilipouliza gharama za sherehe zile nikaambiwa ni shilingi bilioni 4, nikashangaa, bilioni 4 zote ni za nini?" Amesema Rais Magufuli.

Kuhusu sababu za kuruhusu mwaka huu sherehe hizo zifanyike, Rais Magufuli ametaja sababu mbili ambazo ni pamoja na kutumia gharama ndogo huku  sababu ya pili akiitaja kuwa ni kutokana na kwamba hizi ni sherehe za mwisho za Uhuru kufanyika Jijini Dar es Salaam huku akieleza kuwa kuanzia mwaka 2017, sherehe hizo zitakuwa zikifanyika katika makao makuu ya nchi Dodoma.

"Mwaka huu gharama ni ndogo, hata kula wala kunywa hakuna, baada ya hapa hakuna kula wala kunywa"

Rais Magufuli pia ametumia nafasi hiyo kuelezea mafanikio ya Tanzania katika miaka yake 55 ya Uhuru, huku akieleza mikakati ya serikali yake ya awamu ya tano katika kuifikisha nchi kwenye kipato cha kati na kuwashukuru viongozi wakuu wa awamu zilizopita.

Kaulimbiu ya sherehe hizo kwa mwaka huu ni: Tuunge mkono jitihada za kupinga rushwa na ufisadi na tuimarishe uchumi wa viwanda kwa maendeleo yetu
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment