Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Mohamed Utali ametoa agizo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Florent Kyombo kutomhamisha mwalimu yeyote kwa kigezo cha cheti cha ndoa.
Alisema baadhi wanaghushi vyeti hivyo na vya maradhi ili wapate nafasi ya kufundisha kwenye shule zilizopo kando mwa barabara kuu na mijini hivyo kusababisha shule zilizopo mbali kukosa walimu. Utali alisema hayo jana alipofungua baraza la madiwani.
Alisema shule zilizofanya vibaya kwenye matokeo ya darasa la saba ni zilizopo mbali na barabara kuu na zenye upungufu wa walimu.
Mkuu huyo wa wilaya ambaye kitaaluma ni mwalimu alisema anafahamu mbinu na ujanja wanaofanya baadhi ya walimu wanaotaka kufundisha shule za barabarani.
“Mwalimu atakayekuja na kimemo cha kiongozi, ama cheti cha ndoa au ugonjwa na kuomba afundishe shule iliyopo kando mwa barabara kuu usikubali kumhamisha, tutumie madaktari tuwapime tujue hayo maradhi yao,” alisema Utali.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Jonas Van Zeland alimtaka mkurugenzi kuwafuatilia walimu watoro na wanaoshindwa kukaa jirani na shule wanazofundisha kwa madai kuwa mazingira siyo rafiki.
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Kyomba alisema katika matokeo ya darasa la saba mwaka huu, Wilaya ya Mvomero imeshika nafasi ya sita kimkoa na shule zilizofanya vibaya ni zenye uhaba wa walimu.
Alisema atahakikisha anafanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye shule hizo na kuwaomba wazazi, walezi na viongozi wengine wa kata na vijiji, pamoja na madiwani kumpa ushirikiano
0 comments :
Post a Comment