Pamoja na hekaheka za zinazotawala vituo vingi vya mabasi, lakini mtoto Ibrahim Dickson, ndio makazi yake.
Mtoto Ibrahim Dickson (11) ambaye amekuwa akiishi kituo kipya cha mabasi Tabora mjini, kwa kipindi cha miaka minne, ameiomba serikali ya mkoa kumsaidia kurejea kwao Mbeya, pamoja na kumpeleka shule ili aweze kupata elimu.
Dickson, ambaye anajulikana zaidi kwa jina la Wambeya, amekuwa akiishi kituoni hapo baada ya kutelekezwa na mama yake mdogo eneo hilo, ambapo kwa sasa limegeuka kuwa makazi yake ya kudumu.
Kwa mujibu wa Mwandishi wa Azam TV, Juma Kapipi, aliyezungumza na mtoto huyo, anasema kwa sasa Dickson amechoshwa na maisha hayo ya kutangatanga na huku akilalama kupata tabu ikiwemo kupigwa na baridi kali, kipigo kutoka kwa vijana wakubwa, upatikanaji wa chakula, pamoja na mvua na jua vyote vikimhusu.