WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amepokea fedha taslimu sh. milioni 10 kutoka
Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT) zikiwa ni
msaada kwa ajili ya watu waliopatwa na maafa kutokana na tetemeko la
ardhi mkoani Kagera.
Makabidhiano
ya mchango huo yamefanyika leo mchana (Alhamisi, Oktoba 22, 2016)
kwenye Makazi ya Waziri Mkuu, Oysterbay, jijini Dar es Salaam.
Akikabidhi
mchango huo, Askofu Mkuu wa Kanisa la EAGT, Dk. Brown Mwakipesile
amesema kanisa hilo limeona lina wajibu wa kuisadia Serikali
kuwapunguzia machungu watu waliopatwa na maafa kutokana na tetemeko la
ardhi lililotokea mkoani Kagera, Septemba 10, mwaka huu na kusababisha
vifo vya watu 17.
“Tumeona
ni vema kanisa la EAGT lishiriki kuisadia Serikali kuwafariji wananchi
waliopata maafa kutokana na tetemeko hilo. Tumeona ni wajibu wetu kwa
sababu waliopatwa na maafa ni watu wetu wote. Tunawaombea wote
waliopatwa na shida waweze kupata nafuu mapema zaidi,” amesema.
Askofu
Mkuu Dk. Brown ametumia fursa hiyo kuipongeza Serikali kwa kusimamia
vema suala hilo tangu lilipotokea hadi sasa na kuongeza kuwa wanamuomba
Mwenyezi Mungu awape nguvu viongozi wa Serikali ya awamu ya tano ili
waweze kutimiza majukumu yao ipasavyo.
“Ukiacha
hili la tetemeko, tumeona jinsi Serikali ilivyosimamia vizuri suala la
madawati hadi sasa kuna baadhi ya maeneo wamevuka hadi malengo.
Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Magufuli na Serikali nzima kwa kusimamia
jambo hilo vizuri,” amesema.
Amesema
kanisa hilo linatoa shukrani nyingi kwa Mheshimiwa Rais Dk. John Pombe
Magufuli kwa jitihada zinazofanywa na Serikali yake kukabili mambo
mbalimbali yanayowagusa wananchi walio wengi.
Akitoa
shukrani kwa Baba Askofu Mwakipesile na viongozi wa kanisa hilo
aliombatana nao, Waziri Mkuu ameahidi kuwa Serikali itahakikisha
michango hiyo inafikishwa Kagera kwa walengwa. “Nawashukuru sana kwa
jinsi mlivyoguswa na kuamua kuwachangia wenzetu waliopatwa na maafa,
tutahakikisha inawafikia walengwa,” amesema.
Waziri
Mkuu amesema anawashukuru sana viongozi wa dini zote kwa jinsi
wanavyoisadia Serikali kuwahudumia wananchi kupitia sekta mbalimbali.
“Tunatambua juhudi zinazofanywa na taasisi za dini zote kuunga mkono
juhudi za Serikali, tunafarijika mno na tunawashukuru sana,” ameongeza.
Amemuomba
Askofu huyo pamoja na viongozi wengine wa dini wawaombee kwa Mungu
viongozi waliopo madarakani ili awape hekima na busara na awawezeshe
kuwaongoza vema Watanzania.
Tetemeko
hilo la ardhi liliharibu miundombinu ya barabara, shule, zahanati na
kujeruhi watu 440. Pia lilisababisha nyumba 2,063 kuanguka huku nyingine
14,081 zikiwa katika hali hatarishi na 9,471 zikipata uharibifu mdogo
huku wananchi 126,315 wakihitaji misaada mbalimbali.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
0 comments :
Post a Comment