Mashitaka
10 yaliyofunguliwa na walei 32 wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar
es Salaam yakiwemo ya ufisadi wa mali za kanisa, yamesababisha Askofu
Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dk Jacob Chimeledya kumvua uaskofu
Mkuu wa Dayosisi ya Dar es Salaam Dk Valentine Mokiwa.
Hata hivyo Dk Mokiwa amegomea uamuzi huo kwa maelezo kuwa mwajiri wake ni Sinodi ya Dar es Saalam ambayo ndiyo yenye uamuzi wa kumfuta kazi na sio askofu mkuu au askofu mwingine yeyote wa kanisa la Anglikana Tanzania.
Uamuzi
wa kumvua uskofu ulichukuliwa juzi na Askofu Chimeledya baada ya Askofu
Mokiwa kugoma kujiuzulu kama ilivyoshauriwa na nyumba ya maaskofu
ambayo ilimkuta na hatia ya kufuja mali za kanisa hilo na kukiuka
maadili ya kichungaji ambayo yalibainishwa kwenye ripoti ya uchunguzi
iliyoundwa na kiongozi mkuu wa kanisa hilo nchini.
Habari
zilizopatikana kutoka ndani ya kanisa hilo zilieleza kuwa katika kikao
kilichofanyika juzi kanisani Ilala, askofu Chimeledya na ujumbe wake
walihudhuria kikao cha halmashauri ya kudumu ya dayosisi ya Dar es
Salaam akatangaza uamuzi wa kumvua uaskofu Dk Mokiwa chini ya ulinzi wa
polisi.
Licha
ya uamuzi wa kumvua uaskofu, Dk Chimeledya pia aliagiza waraka
unaoagiza askofu huyo kuondolewa madarakani, usambazwe kwenye makanisa
yote yaliyoko chini ya dayosisi ya Dar es Salaam na usomwe jana kwenye
ibada mbele ya waumini.
“Ni
kweli kikao hicho kilifanyika jana, Dk Chimeledya alikuja na katibu
mkuu na msajili wa kanisa kwenye kikao, lakini tulishangaa kwamba
walikuja na askari polisi kinyume na utaratibu wa kanisa, alisoma
maamuzi hayo aliyodai yametolewa na nyumba ya maaskofu,”alisema msemaji wa Dayosisi ya Dar es Salaam Yohana Sanga.
Dk Mokiwa agoma kung’oka
Katibu
Mkuu wa Dayosisi ya Dar es Salaam Padri Jonathan Senyagwa jana alisema
habari hizo sio za kweli na barua ambazo zimesomwa katika baadhi ya
makanisa jijini Dar es Salaam zilisomwa kwa makosa.
“Mwenye
mamlaka ya kumfukuza kazi ni yule aliyemwajiri, na mwajiri wa Dk Mokiwa
ni Sinodi ya Dar es Salaam...tutatoa tamko hivi karibuni kuthibitisha
kwamba askofu wa jimbo bado hajafukuzwa,” alisema Padri Senyagwa.
Alisema
waraka ambao umesambazwa na askofu mkuu wa Tanzania haujapitia kwenye
halmashauri ya kudumu ya dayosisi ili kupata baraka zake na wala hauna
baraka kutoka kwa sinodi ya dayosisi jambo ambalo linaufanya waraka huo
ukose sifa za kutekelezeka.
“Ninachokwambia
ni kwamba askofu wa dayosisi ya Dar es Salaam bado ni Mokiwa,
hatuzitambui barua zilizosomwa katika baadhi ya makanisa,” alisisitiza katibu mkuu huyo wa Dayosisi.
Mgomo
huo pia ulithibitishwa na Sanga, ambaye alifafanua kuwa juzi
kulifanyika kikao kati ya viongozi wakuu wa kanisa na halmashauri ya
kudumu ya dayosisi ya Dar es Salaam na kuelezwa na askofu mkuu wa
Tanzania Dk Chimeledya hatua ya kumvua uaskofu Dk Mokiwa jambo ambalo
halmashauri iligoma.
“Tulifanyia
kikao chetu pale kanisa la Ilala, viongozi wetu wakuu walikuja na
polisi wakatusomea huo waraka na kutangaza maamuzi hayo mbele ya
halmashauri, lakini maamuzi hayo yaligomewa na wajumbe wa halmashauri ya
Dayosisi ya Dar es Salaam,” alisema Sanga.
Alisema halmashauri iligoma kubariki uamuzi huo kwa sababu kanisa la Anglikana Tanzania lina kanuni na taratibu zake.
Alifafanua
kuwa waraka wa kumwondoa madarakani Dk Mokiwa lazima upate baraka za
halmashauri ya kudumu ya dayosisi na sinodi ya dayosisi.
“Ule
waraka tuliupitia na kubaini kuwa hauna baraka za nyumba ya maakofu,
wala hauna baraka za halmashauri ya kudumu na Sinodi ya dayosisi ndio
maana tuliwakatalia,” alisema Sanga na kuongeza kuwa maamuzi ya
kumvua uaskofu Dk Mokiwa yamefanywa na askofu mkuu wa Tanzania, katibu
mkuu na msajili wa kanisa na sio vikao vya kanisa.
“Ninachosisitiza
hapa ni kwamba askofu wa dayosisi ya Dar es Salaam bado ni Dk Mokiwa,
huo waraka uliotangazwa ni ushawishi wa watu wachache wanaotaka
kumchafua kiongozi wetu wa Dayosisi,” alisema.
Aombwa ajiuzulu uaskofu
Awali
tume hiyo iliyoundwa kuchunguza tuhuma dhidi yake, baada ya kubaini
makosa mengi yaliyofanywa na askofu huyo ilimshauri ajiuzulu wadhifa
wake na awe tayari kufanya huduma nyingine ya kumtumikia Mungu.
“Hatua
tunayoichukua ni kwa nia njema kabisa ya kulinusu kanisa letu ambalo
limekuwa naheshima kubwa hapa nchini na duniani kote,” unasema waraka uliosaniwa na Dk Chimeledya.
Tume hiyo ilichukua uamuzi huo katika kutatua mgogoro uliopo ndani ya dayosisi ya Dar es Salaam:
“Nia
yetu ni njema kabisa na hatuna chuki, uhasama wala upendeleo katika
jambo hili, ifahamike kuwa vyombo vyote ndani ya kanisa ikiwemo nyumba
ya maaskofu vinalifahamu jambo hili vyema, hivyo tulitarajia tutaungwa
mkono ili kuisaidia dayosisi yetu ya Dar es Salaam kwenda mbele.”
Pia
waraka huo unaeleza kuwa hiyo sio mara ya kwanza kanisa hilo kufanya
maamuzi ya namna hiyo na kutoa mfano kuwa hata enzi za askofu Mokiwa
akiwa askofu mkuu wa Tanzania alichukua hatua za kulinusuru kanisa
lisipotee katika migogoro mbalimbali ikiwemo mgogoro wa dayosisi ya
Tanga ambako alimtaka askofu wa dayosisi hiyo ajiuzulu kwa hiyari na
alikubali.
Baada
ya kutenguliwa uaskofu wa Mokiwa, Dayosisi ya Dar es Salaam itakuwa
chini ya uangalizi wa uongozi wa askofu mkuu mpaka taratibu nyingine za
kikanuni zitakapokamilika.
“Nina
wasii Wakristo wote kwa nieaba ya Bwana Yesu Kristo tuendelee kuwa
watulivu katika kuijenga dayosisi yetu na kanisa la Mungu kwa ujumla.”
Mashitaka 10 ya Mokiwa
Askofu
Mokiwa Machi 2015 alifunguliwa mashitaka 10 ambayo ni kuizuia dayosisi
ya Dar es Salaam kupeleka michango pasipo maelekezo ya sinodi ya
Dayosisi ya Dar es Salaam, kuhamasisha dayosisi kujitoa katika udhamini
wa kanisa Anglikana Tanzania (KAT) kwa lengo la kuifarakanisha dayosisi
na jimbo kinyume na katiba ya dayosisi.
Mashitaka
mengine ni kufuja mali za kanisa na kuingia mikataba kiholela yenye
viashiria vya rushwa katika eneo la kanisa la mtoni Buza na miradi
mingine, kushindwa kutatua migogoro inayohusu uwekezaji na maadili baina
ya dayosisi na mitaa ya Magomeni ambao kuna mgogoro na Benki ya DCB,
kanisa la Kurasini na mengine.
Askofu
huyo pia anadaiwa kushindwa kutatua migogoro baina ya mapadiri na
waumini na kutunza mali za kanisa katika mtaa wa Watakatifu wote Temeke
na kutelekeza nyumba ya askofu iliyopo Oysterbay ambako imegeuzwa kuwa
yadi ya kuuza magari.
Pia
alilalamikiwa kushitakiwa mahakamani na Marehemu Christopher Mtikila na
watu wengine watatu kwa kosa la kuwatishia silaha ya moto na kuwapapasa
maungoni mwao bila ridhaa yao kinyume na maadili ya kikanisa.
Askofu
Mokiwa pia analalamikiwa kuanzisha taasisi ya MEA Foundation
iliyomwezesha kupokea fedha nyingi za wafadhili kwa ajili ya maendeleo
ya dayosisi, lakini fedha zimefujwa na hesabu za chombo hazikuwahi
kukaguliwa.
Tuhuma
zingine ni kurejea kwa mchakato wa mapitio ya katiba mpya na kuvuruga
mchakato wa awali wa maandalizi ya katiba mpya ya dayosisi kwa kutumia
fedha za dayosisi na kutekelezwa askofu msaidizi dayososi ya Katanga
Kalemi .
0 comments :
Post a Comment