BAADA ya kuwa nje ya ulingo wa siasa takribani
mwaka mmoja, hatimaye mbunge wa zamani wa Nyamagana, Ezekiel Wenje amechaguliwa
kuwa Mwenyekiti wa Chama hicho Kanda ya Ziwa Victoria.
Wenje alitangazwa juzi kupitia uamuzi wa
Kamati Kuu ya Chadema kuwa mgombea uenyekiti wa chama hicho kabla ya kuibuka
mshindi katika uchaguzi uliojumuisha wagombea kutoka mikoa ya Geita, Mwanza na
Kagera yenye majimbo ya uchaguzi 25.
Mbunge huyo wa zamani alikuwa akichuana
na Meya wa Manispaa ya Bukoba Mjini, Chifu Kalumuna ambapo katika uchaguzi huo
uliofanyika juzi saa tatu usiku, Wenje aliibuka mshindi.
Hadi juzi jioni wagombea wanne ndio waliotajwa
kuwania nafasi hiyo, akiwamo aliyewahi kuwa Mhariri Mtendaji wa Gazeti la
Tanzania Daima, Ansbert Ngurumo, ambaye katika uchaguzi huo alihamishiwa
kugombea nafasi ya Umakamu Mwenyekiti na kuibuka mshindi.
Awali, wagombea wengine wa nafasi hiyo
akiwamo aliyekuwa Mwenyekiti wa Kanda hiyo, Peter Makere na Ofisa wa Chama
hicho, Tungaraza Njugu waliondolewa kuwania nafasi hiyo.
Akizungumzia kuchaguliwa kwake kushika
nafasi hiyo, Wenje alisema: “Nitafanya kazi kwa kushirikina na viongozi
wenzangu kuhakikisha tunaijenga Kanda ya Ziwa. Tutahakikisha tunashinda katika uchaguzi
ulio mbele yetu, kasi yangu niliyokuwa nayo nitaendelea nayo hiyo hiyo.”
Itakumbukwa kuwa katika uchaguzi wa
mwaka jana, Wenje aliyekuwa na nguvu katika jimbo la Nyamagana aliangushwa na
Stanslaus Mabulab wa CCM.
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Viti
Maalumu Mwanza, Suzan Masele aliyekuwa akigombea nafasi ya uhazini aliangusha
na Bugomba Mzuba.
0 comments :
Post a Comment