Fahamu undani Wa Faida Juu Ya Mradi Wa Dart



 SIKU moja baada ya Rais John Magufuli kutaka apelekewe taarifa za faida ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (Udart), Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, ameshindwa kueleza faida za mradi huo.


Akizungumza juzi katika uzinduzi wa mradi huo wa awali, Rais Magufuli alishangaa hotuba zote zilizotolewa katika uzinduzi huo, ikiwamo ya Simbachawene na ya Waziri Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, kushindwa kueleza faida ya mradi huo.

Kutokana na kasoro hiyo, Rais Magufuli aliagiza apelekewe taarifa za faida ya mradi huo unaotoa  huduma kwenye barabara ya Morogoro, kwa kuwa umejengwa kwa mkopo wa Sh bilioni 403, ambazo zinatakiwa kulipwa na kuonya kuwa akiletewa taarifa ya hasara, atatumbua wahusika.

Waziri

Akizungumzia agizo hilo jana, Waziri Simbachawene alitoa taarifa za mapato tu, bila kueleza gharama za uendeshaji na kukiri kuwa hawezi kuzungumzia faida au hasara za mradi, kwa kuwa inahitaji mjadala.

“Ni suala la kukaa chini na kujadiliana, huwezi kusema tu hasara, ndiyo maana mimi nimejaribu kutoa mwelekeo wa makusanyo na mapato, sasa ni ngapi, zimekuwaje, zimefanyikaje ni suaala la kimahesabu,” alisema Simbachawene.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, mradi huo ulipoanza Mei mwaka jana makusanyo kwa mwezi yalikuwa Sh milioni 800, baadaye yakapanda hadi Sh bilioni moja kwa mwezi, ikaendelea hadi Sh bilioni mbili na hadi Desemba, mradi ulikuwa umeingiza zaidi ya Sh bilioni 19.

Misuguano

Hata hivyo, alisisitiza kuwa hawezi kuwa tayari kutoa mahesabu, kwa kuwa biashara yenye wabia wengi, lazima iwe na misuguano ambayo inapaswa kufanyiwa uchambuzi na kupata jibu moja.

“Unapokuwa na biashara yenye wabia wengi si jambo jepesi la kudhani inaweza ikawa imekuwa moja jumlisha moja sawa na mbili, lazima kuwepo misuguano, huyu anasema hivi na yule anasema vile, lakini hayo sasa tunaweza kufanya uchambuzi na kutoka na jibu moja,” alisema.

Simbachawene alisema jambo kubwa na la msingi ni kwamba Dart wanalipwa chao, Sh milioni 8.1 kwa siku, kwa ajili ya matumizi ya miundombinu.

“Tumeona bora ya huo mfumo kuliko kuingia kwenye mahesabu, kwa hiyo mwanzo walikuwa wanalipwa Sh milioni 4.4 kwa siku, Bodi yangu ikanishauri, tukafanya uchunguzi.

“Baada ya uchunguzi wakasema hapa tunaweza kufanya hiki, hivyo kwa sasa mradi ule unailipa Dart Sh milioni 1.8 bila kukosa na inakatwa kwenye mfumo.

“Sasa unajiuliza je, Dart na wenyewe kwa matumizi ya Sh milioni 8.1 kwa siku, ukipiga mara 30 inapata Sh milioni 200 na zaidi je, wanaweza kujiendesha au kulipa mishahara na mambo mengine? Unaona hii inawezekana,” alisema.

Matarajio
Alisema mradi huo unaweza kujiendeshwa vizuri na hadi sasa  una abiria 200,000 kwa siku,  lakini wakipata abiria 450,000  watapata fedha nyingi na kurudisha gawio serikalini.

Akifafanua, Simbachawene alisema hapo alizungumzia fedha inayopelekwa Dart tu, lakini bado asilimia 41 zilizo kwenye uendeshaji za Simon Group, kwa kuwa Serikali pia ina asilimia 49 na Simon Group ina asilimia 51.

Kutokana na hisa hizo 49 za Serikali, Simbachawene alisema kuna gawio na kwamba fedha za gawio pia zinaingia serikalini kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, ambapo ikijumilishwa na inayokwenda Dart, inakuwa si haba.

Waziri alisema hayo bila kuchanganua gharama za mradi ili kubaini faida, wakati juzi Rais Magufuli alionya kuwa tangu alipoanza kutambua biashara, hajawahi kuwa na tafsiri inayoonesha hasara.

Mradi huo ambao kwa mujibu wa matarajio ya Rais Magufuli, unapaswa kuwa wa faida, ni awamu ya kwanza, kwa kuwa awamu zingine zinafuata ili kuondoa hasara ya Sh bilioni 411.55 wanayopata wananchi kwenye foleni za Dar es Salaam kila mwaka.

Awamu zingine zitakazojengwa miundombinu ya mabasi ya kasi na kuanza kutoa huduma hiyo ni kutoka Gerezani, Kariakoo mpaka Mbagala Rangi Tatu, kwa awamu ya pili.

Awamu ya tatu ni kutoka barabara ya Bibi Titi Mohamed hadi Gongo la Mboto, huku awamu ya nne ikihusu barabara ya Ali Hassan Mwinyi kwenda Bagamoyo, kipande chenye urefu wa kilometa 25.

Katika awamu ya tano, miundombinu hiyo itajengwa na huduma kuanza kutolewa kwenye kipande cha kilometa 22.8 barabara ya Mandela, huku awamu ya sita na ya mwisho ikihusu barabara ya Mwai Kibaki yenye kipande cha kilometa 27.6.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment