Kocha mpya wa Azam
FC, Mromania, Aristica Cioaba, kwa mara ya kwanza Jumamosi ijayo
anatarajiwa kukaa katika benchi kuiongoza timu hiyo itakapopambana na
Simba kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa Uwanja wa Uhuru, Dar.
Mromania huyo ambaye
amepewa mkataba wa miezi sita na Azam akichukua nafasi ya Mhispania,
Zeben Hernandez aliyetimuliwa mwishoni mwa mwaka jana, bado hajaanza
kazi rasmi ya kuinoa timu hiyo kutokana na kukosa kibali cha kufanyia
kazi hapa nchini.
Meneja wa timu hiyo,
Philip Alando, amesema: “Kila kitu tumekamilisha kwa maana ya kulipia
gharama za kupata kibali, kilichobaki kwa sasa ni kusubiri tu uhamiaji
kuona ni lini watatupatia hicho kibali.
“Kwanza tumeomba
kibali cha kazi, tutakapokipata, ndipo tutafanya mchakato wa kuomba
kibali cha makazi, matarajio yetu ni kuona kabla hatujapambana na Simba
tumekamilisha kila kitu ili kocha wetu huyu aanze rasmi kazi.”
Ikumbukwe kuwa, kwa
sasa kikosi cha Azam kinanolewa na kocha wa muda, Idd Nassor Cheche
baada ya Zeben na benchi lake la ufundi lililokuwa likiundwa na
Wahispania watano kufutwa kazi kutokana na matokeo mabaya waliyokuwa
wakiyapata.
0 comments :
Post a Comment