Aliyekuwa
mgombea urais Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Maalim
Seif Sharif Hamad, amesema yupo tayari kufanya tena maridhiano endapo
pande zote mbili zitakubali kwamba Zanzibar kuna matatizo.
Maalim
Seif aliyasema hayo jana katika kipindi cha Funguka kinachorushwa na
Televisheni ya AZAM na kuongozwa na mtangazaji nguli nchini, Tido
Mhando.
Alisema
maridhiano yaliyofanyika akiwa na Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dk. Amani
Abeid Karume, yalikuwa na manufaa makubwa kwa kuwa Zanzibar ilikuwa na
amani na utulivu.
Maalim
Seif alisema CUF iliamua kukaa na Karume baada ya kuona uchaguzi
ulikuwa unakaribia kufanyika hivyo ikaamua kufanya kikao cha muafaka wa
maridhiano na kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) iliyozaa
matunda.
Alisema
baada ya kufanyika maridhiano na kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais alikuwa
na nafasi kubwa ya kumshauri Rais mambo mbalimbali.
“Hata
kulipokuwa na SUK (Serikali ya Umoja wa Kitaifa), mambo yalikuwa
mazuri na maelewano na hata ilikuwa ikitokea mtu akifika ofisini
anashindwa kufahamu CUF ni nani na CCM ni nani,’’ alisema Maalim Seif.
Alisema
hata sasa kama kuna nia njema ya kufanyika mazungumzo yafanyike kwa
sababu kwa sasa Zanzibar kuna matatizo na uhasama unazidi kupamba moto.
Maalim
Seif pia alizungumzia suala la kufutwa Uchaguzi Mkuu uliofanyika
Oktoba 25, mwaka 2015 na marudio yake Machi 20 mwaka jana.
Alisema
yeye alishinda kwa kura nyingi na hivyo kama uchaguzi ungekuwa huru na
haki yeye ndiyo alistahili kutangazwa kuwa Rais wa Zanzibar na si
vinginevyo.
Alisistiza
kwamba hatambui uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20, mwaka jana
kwa kuwa hakushiriki na wala hakuwa na sababu ya kushiriki kwa kuwa
mshindi alishapatikana Oktoba 25, mwaka juzi.
“Nisingeweza
kukubali kurudia uchaguzi ule kwa kuwa mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi
(ZEC) alifuta matokeo yale ili CCM kwa njia zozote zile ishinde kwenye
uchaguzi wa marudio.
“Hawakuweka mpira uwanjani urudiwe eti kwa sababu washindwe si kweli, hivyo wangetumia mbinu zozote ili washinde ,’’alisema Maalim Seif.
Seif
ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, alisema ni kosa kukaa kimya wakati
bado suala la uchaguzi linafanyiwa kazi ili ufumbuzi upatikane.
Alisema hilo ni kama bomu ambalo likiripuka hali itakuwa mbaya.
Mtangazaji alimuuliza MaalimSeif kama hakuona kuwa ni kosa kujitangazia ushindi?
Alisema
alifanya hivyo baada ya kuona kwamba ZEC ilikuwa anataka kumtangaza Dk.
Shein (Ali Mohamed Rais wa Zanzibar) kuwa ni mshindi huku hakushinda.
Hata hivyo alisema kama waliona amefanya makosa basi wangemkamata na kumpeleka mahakamani.
Alisema bado ana matarajio ya kuwa Rais wa Zanzibar katika muda mfupi ujao.
Kuhusu uchaguzi wa 2020, alisema ataangalia hali ya siasa ijayo.
Mgogoro ndani ya CUF
Akizungumzia mgogoro ndani ya chama hicho, alisema unachangiwa na Msajili wa Vyama vya Siasa.
Alisema
Profesa Ibrahimu Lipumba aliamua kuondoka yeye mwenyewe. “Lakini cha
kushangaza baada ya miezi 10 akarudi sijui ni kwa misingi gani?”
alihoji.
Alisema
Katiba iko wazi kwa mtu anayejiuzuru, ni kwamba anaandika barua kwa
Katibu Mkuu na Katibu anapeleka barua kwenye Mkutano Mkuu.
Alipoulizwa
mbona alipokabdhiwa barua hakuitisha mkutano wa kumridhia Lipumba
kujiuzulu, alisema hawakuweza kuitisha mkutano ghafla kwa kuwa chama
hicho ni kidogo na hakikuwa na fedha.
‘’Lakini
tuliitisha Mkutano Mkuu akajadiliwa, cha kushangaza yeye anang’ang’ania
kuwa ni mwenyekiti, hii inashangaza haiwezekani katika hili!’’ alisema.
Alisema hata Msajili anafahamu kurudi kwa Lipumba ni lazima akubaliwe na Mkutano Mkuu.
Hata
hivyo, alisema katiba ya chama haisemi mtu anayeondoka akae na baadaye
aamue kurudi kwa sababu hawafahamu kama ana nia njema na chama au la
ikizingatiwa pia alikiacha chama katika kipindi kigumu cha uchaguzi
mkuu.
Seif
alisema kutokana na Msajili wa Vyama vya Siasa kuendelea kumtambua
Profesa Lipumba licha ya kujiuzuru yeye mwenyewe, CUF kimeamua kwenda
mahakamani kuweza kupata tafsiri ya sheria.
“Mgogoro
huu ulipandikizwa kwa wazi kabisa na Lipumba wakati anajiuzuru
tulimfuata na viongozi mbalimbali, wa dini wa chama wazee na vijana
asitoke lakini alikataa kuendelea kubaki kwenye nafasi hiyo,’’ alisema.
Maalim
Seif alisema kwa kufanya hivyo imeonekana kuwa Lipumba hakuwa na
msimamo kwa kuwa yeye ndiye aliyewaletea aliyekuwa mgombea urais
akiwakilisha Ukawa, Edward Lowassa, huku akisema kuwa kila alipokuwa
akipita vijiweni, Lowassa alikuwa akitajwa tajwa sana na wananchi.
Alisema
yeye na wenyeviti wenzake wa Ukawa walimtangaza Lowassa, hivyo
Lipumba kubadili msimamo kulionyesha dhahiri kwamba tayari kulikuwa na
nguvu nyuma yake iliyokuwa ikimshawishi na hata baada ya kujiuzuru
iliendelea kufanya hivyo.
Maalim
alisema baada ya Lipumba kukaa pembeni CUF kilipata mafanikio makubwa
kwa vile kilipata viti vya ubunge 10 upande wa Bara na halmashauri nne
ambazo ziliundwa na chama hicho peke yake.
Alisema
hata katika uchaguzi mdogo wa marudio wa hivi karibuni, Lipumba
alisimamisha wagombea katika kata 11 lakini hakuambulia kiti hata kimoja
zaidi ya wagombea kupata kura 10 ,11,12.
Alipoulizwa
hatima ya CUF kwa sasa, alisema hiyo si mara ya kwanza kwa vile kuna
migogoro mikubwa ilipita huko awali ukiwamo wa Hamad Rashid Mohamed
lakini ulikwisha.
Kuhusu kama ana mpango wa kuunda chama kingine, alisema ni hisia za watu tu na kwamba hana mpango huo.
Alisema yeye ni mmoja wa waanzilishi wa CUF akiunda chama kingine ataonekana kuwa ni msaliti.
“Siwezi kuunda chama kingine nikaachana na CUF, mimi ni CUF kindakindaki na nitaendelea kuwa CUF kindakindaki ndani ya chama ,’’alisema.
Alisema
CUF kimeamua kupeleka mahakamani mgogoro huo na hata kama mahakama
itampa Lipumba ushindi watakata rufaa ingawa hawatarajii hilo.
Maalim
Seif alikiri kwamba bila vyama vya upinzani kuungana ni vigumu
kukiondoa CCM madarakani na ndiyo sababu ya kufanya hivyo.
Mgogoro wa ruzuku
Alimshangaa
Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kutoa ruzuku kwa Profesa Lipumba
kupitia akaunti nyingine ambayo si ya chama makao makuu.
Alisema
Msajili aliwaandikia barua kusema kuwa ruzuku isingetolewa kutokana na
chama hicho kuwa na mgogoro, lakini baada ya muda wakashangaa
imepitishiwa katika akaunti ya wilaya ya Temeke.
Kuhusu
kushindwa uchaguzi wa marudio, Dimani alisema siyo kwamba wameshindwa
bali Dimani ni jimbo la CCM na hata hivyo kama demokrasi CCM
ingetumika isingeshinda.
Maisha baada ya kustaafu
Maalim Seif alisema licha ya kustaafu anapata haki zake zote kisheria siyo kuomba.
Haki
hizo ni pamoja na gari, walinzi na posho kila mwezi ingawa alisema
matibabu anajigharamia mwenyewe kwa kuwa akiomba ananyanyaswa.
Msikilize zaidi Kwenye video hii....
0 comments :
Post a Comment