Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 13 Januari, 2017 ameyaonya magazeti
mawili yanayoandika habari za uchochezi na kupotosha wananchi kwa kuwa yanahatarisha amani ya nchini.
Rais Magufuli ametoa onyo hilo wakati akikagua na kufungua Kiwanda cha Jambo cha kuzalisha vinywaji baridi mkoani Shinyanga.
Rais Magufuli amesema Serikali
haitayavumilia magazeti hayo mawili kwa kuandika habari za uchochezi
ambazo zinaweza kuhatarisha amani ya nchi kama ilivyotokea katika nchini
ya Rwanda na kupelekea mauaji ya kimbari nchini humo.
”Serikali ya kutumbua majipu haiwezi
kuacha kutumbua magazeti yanayofanya mambo ya uchochezi hatuwezi kuiacha
Tanzania ikawa dampo la eneo la kuweka maneno ya uchochezi chini ya
utawala wangu hilo halitakuwepo kuna magazeti mawili tu kila ukisoma wao
ni kuchochea tu ikizungumzwa habari hii wao wanageuza hii nasema na
nataka wanisikie siku zao zimeshafika kama wanasikia wasikie wasiposikia
wasisikie lakini magazeti mengine na vyombo vyote vingine vinatoa
uchambuzi mzuri sana”.
Rais Magufuli amesema Serikali yake
haiwezi kuvumilia kuona amani ya nchi inahatarishwa na magazeti mawili
kwani amani ndio chimbuko la maendeleo ya taifa lolote duniani.
Amesema bila kuwepo kwa amani hakuna
mwekezaji atakayeweza kuja kuwekeza nchi, hata wawekezaji wa ndani
watashindwa na hivyo kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.
Rais Magufuli amesema uwepo wa amani
nchini ndio uliowezesha wawekezaji wa Kiwanda cha Fresho cha
kutengenezea mifuko ya kubebea bidhaa za chakula nchini na kiwanda cha
Jambo cha kuzalisha vinywaji baridi mkoani Shinyanga kujengwa mkoani
hapo kwani bila amani visingeweza kujengwa.
Aidha ameitaka Benki ya Uwekezaji Nchini
TIB na Taasisi nyingine za fedha kutoa mikopo kwa wawekezaji wanaotaka
kuwekeza katika viwanda badala ya kuwakopesha wanasiasa ambao hutumia
fedha wanazokopa kwa matumizi yasiyowanufaisha watanzania waliowengi
Rais Magufuli ameupongeza uongozi wa mkoa
wa Shinyanga kwa kuanza kutekeleza kwa vitendo azma ya Serikali ya
kutaka Tanzania ya viwanda kwa kujenga viwanda vingi mkoani humo ikiwa
ni pamoja na viwanda hivyo viwili alivyovizindua katika siku yake ya
mwisho ya ziara mkoani Shinyanga.
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano, Ikulu
Shinyanga
13 Januari 2017.


0 comments :
Post a Comment