Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya
Taifa ya Uchaguzi Bw. Ramadhani Kailima akitoa Ufafanuzi kuhusu
malalamiko ya ukiukwaji wa maadili ya Uchaguzi yaliyotolewa na Chama cha
ACT WAZALENDO.
……..
Na. Aron Msigwa –NEC, Dar es Salaam.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
imekishauri Chama cha ACT – Wazalendo na Vyama vingine vyenye wagombea
wa Ubunge katika Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Dimani na Udiwani katika
Kata Ishirini (20) za Tanzania Bara ,kuwasilisha malalamiko ya ukiukwaji
wa Maadili ya Uchaguzi kwenye Kamati za Maadili zilizo katika maeneo
yao.
Akizungumza na vyombo vya habari
leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC), Bw. Kailima Ramadhan amesema NEC imepata taarifa kupitia
Vyombo mbalimbali juu ya malalamiko ya Chama Cha ACT-Wazalendo
kuvilalamikia Vyombo vya Dola pamoja na Watendaji wa Umma kufanya
vitendo vyenye muelekeo wa kukipendelea Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Bw. Kailima amefafanua taarifa ya
Chama hicho iliyotolewa kwenye Vyombo vya Habari Januari, 12 2017,
imeeleza kuwa Watendaji wa Halmashauri ya Geita waliwakusanya Wazee
katika Kata ya Nkoma waje na Vitambulisho vyao vya kupigia Kura kwa
lengo la kuwapatia huduma ya afya bure jambo linalolalamikiwa na ACT-
Wazalendo kwa madai kwamba Watendaji hao wana lengo la kuwahadaa Wazee
hao ili wakipigie Kura Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Aidha, amesema katika malalamiko
yake Chama cha ACT Wazalendo kimeibua tuhuma za wananchi kupokwa kadi za
kupigia Kura ili wasiweze kushiriki katika uchaguzi mdogo utakaofanyika
Januari 22, 2017.
Mkurugenzi Kailima amesisitiza
kuwa ni kosa chini ya kifungu cha 88 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi,
Sura ya 343 na kifungu cha 100 cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za
Mitaa, Sura ya 292 mtu kumiliki kadi ya kupigia kura isiyokuwa yake.
“Natoa wito kwa wananchi wote
kwamba, ni kosa chini ya kifungu cha 88 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi,
Sura ya 343 na kifungu cha 100 cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za
Mitaa, Sura ya 292 mtu yeyote kumiliki kadi ya kupigia kura isiyokuwa
yake” Amesema.
Amefafanua kuwa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi kwa kuzingatia sehemu ya 5.4 ya Maadili ya Uchaguzi
inavikumbusha Vyama vya Siasa kuwa iwapo vitakuwa na malalamiko ya
ukiukwaji wa Maadili ya Uchaguzi katika Uchaguzi Mdogo wa Udiwani
viwasilishe malalamiko hayo kwenye Kamati ya Maadili ngazi ya Kata ndani
ya saa 72 tangu kutokea kwa tukio linalolalamikiwa.
“ Sehemu ya 5.4 ya Maadili ya
Uchaguzi yaliyosainiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Serikali na Vyama Vya
Siasa inaeleza wazi muda wa kuwasilisha malalamiko kwa kuvitaka vyama
au wahusika wenye malalamiko yoyote kuyawasilisha kwa maandishi kwenye
Kamati ya Maadili ya Uchaguzi ya ngazi husika ndani ya saa 72 tangu
kutokea kwa tukio” Amesisitiza Kailima.
Amesisitiza kuwa iwapo Chama cha
Siasa au Mgombea hataridhika na maamuzi ya Kamati ya Maadili ngazi ya
Kata, kwa kuzingatia sehemu ya 5.7 (a) ya Maadili ya Uchaguzi anatakiwa
awasilishe rufaa yake kwa Msimamzi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo ndani ya
saa 24 tangu maamuzi ya Kamati ya Maadili ngazi ya kata kutolewa.
Aidha, Bw. Kailima amebainisha
kuwa kama Chama cha Siasa hakikuridhika na maamuzi ya Kamati ya Maadili
ngazi ya Jimbo, bado kwa kuzingatia sehemu ya 5.7 (b) na (c) kinayo
fursa ya kuwasilisha Rufaa yake katika Kamati ya Maadili ngazi ya Taifa
au ngazi ya Rufaa ambayo ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
“ Tunavishauri Vyama vya Siasa na
Wagombea kuzingatia matakwa ya Maadili ya Uchaguzi katika kuwasilisha
malalamiko yao ya ukiukwaji wa maadili ya Uchaguzi, kwa mujibu wa sehemu
ya 5.7(e) ya Maadili ya Uchaguzi, pale ambapo Chama cha Siasa au
Mgombea hakuridhika na maamuzi ya Kamati ya Rufaa atakuwa na fursa ya
kuwasilisha malamiko yake Mahakamani baada ya Uchaguzi kwa mujibu wa
Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na Sheria ya Uchaguzi ya
Serikali za Mitaa, Sura ya 292”.
Amesisitiza kuwa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi inaendelea kuwasihi viongozi wa Vyama vya Siasa na Wadau
wengine wa Uchaguzi kuendelea na Kampeni za kistaarabu na kuzingatia
Sheria, Kanuni na Maadili ya Uchaguzi na kwamba inaendelea kufuatilia
kwa karibu kila hatua ya Uchaguzi na hasa Kampeni huku akisisitiza kuwa
haitasita kuchukua hatua kwa mtu yeyote atakayekiuka Sheria za Uchaguzi.


0 comments :
Post a Comment