SIKU chache baada ya Idara ya Uhamiaji kukamata raia wa India kwa madai
ya kufanya kazi bila vibali, Balozi wa India nchini, Sandeep Arya,
ameingilia kati suala hilo na kusema tatizo lilikuwa mawasiliano kati ya
mwajiri na Uhamiaji.
Akizungumza jana , Balozi Arya alisema anaendelea kufuatilia kwa karibu
suala hilo na kudokeza kuwa jitihada za kumaliza sintofahamu hiyo,
zinaendelea kwa njia ya mazungumzo kati ya mwajiri na Idara hiyo.
Akifafanua baada kumaliza kikao chake na wawakilishi wa kampuni 30 za
kutengeneza dawa kutoka India zinazojiandaa kuwekeza nchini, Balozi Arya
alisema baada ya kubaini tatizo kuwa mkanganyiko wa mawasiliano, ndiyo
maana wameruhusu kampuni hizo kuwekeza nchini.
“Unajua zipo ajira za muda, zingine miaka miwili, hivyo udhaifu wa
mawasiliano ulisababisha sintofahamu, hivyo taratibu za kufanya ukaguzi
zinapaswa kuchukuliwa na vibali vitolewe maisha yaendelee,” alisema.
Balozi Arya alisisitiza kuwa jitihada za kumaliza sintofahamu hiyo,
zinaendelea kwa njia ya mazungumzo na ofisi yake kwa kushirikiana na
Serikali ya Tanzania, watahakikisha suala hilo linamalizika kidiplomasia
bila kuathiri ushirikiano uliopo.
0 comments :
Post a Comment