Chama
cha Demokrasi na Maendeleo (Chadema), kimesema kipo kwenye maandalizi
ya kumkabidhi kadi mrembo wa Tanzania mwaka 2006, Wema sepetu, pamoja na
kundi lake lenye zaidi ya watu 500.
Wema
alikuwa mmoja kati ya wanachama maarufu wa CCM katika kundi la wasanii
wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka juzi kwa
kaulimbiu ya ‘mama ongea na mwanao’.
Akiwa kama kiongozi wa wasanii, alishiriki kumnadi Mgombea Mwenza wa CCM ambaye kwa sasa ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.
Katika
mkutano wake na wanahabari mwishoni mwa wiki, Wema alisema kwa sasa
ameamua kuvaa magwanda na yupo tayari kwa mapambano.
Mkuu
wa Idara ya Habari wa Chama cha Demokrasi na Maendeleo (Chadema),
Tumaini Makene jana alisema wapo kwenye maandalizi na kabla ya Machi
5, mwaka huu watamkabidhi Wema kadi ya uanachama na kundi lake
linalomuunga mkono.
“Wema atakabidhiwa kadi kwa utaratibu maalumu maana ameonyesha heshima na nia ya kujiunga kwenye mapambano ya kweli.
“Kwa kweli Chadema tunafarijika sana na kuja kwake maana kuna timu kubwa inayomuunga mkono pia wanataka kujiunga na chama.
“Tena
na wengine wanatoka katika mashirikisho mbalimbali ikiwamo TFF. Kwa
hiyo hapo unapata picha ya Wema ni mwanachama mpya wa Chadema mwenye
mvuto wa aina yake na huwezi kubeza hata kidogo kuja kwake,” alisema Makene
Alisema
wakati wowote chama hicho kitatangaza lini mwanachama huyo atakabidhiwa
kadi ya Chadema, tukio ambalo alisema litakuwa la aina yake.
Akizungumza
nyumbani kwao Sinza, Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Wema alisema
amechukua uamuzi wa kuhama CCM baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Paul Makonda, kumtaja katika orodha ya watu wanaotumia dawa za kulevya.
Alisema kitendo hicho kilimdhalilisha kwa kiwango kikubwa.
“Nimeamua
kufanya uamuzi wa kuhama CCM na sasa nahamia Chadema. Sitaki nionekane
labda nimepata hasira kulingana na tuhuma zinazonikabili, lakini nataka
nionekane nimefanya uamuzi kama binadamu yeyote angeweza kufanya.
“Nimekubali
na nimekiri kwamba nilisema nitakufa nikiwa CCM lakini ya Mungu mengi.
Natamani ningejua awali, nasema sijachelewa, naamini uamuzi wangu
nilioufanya ni sahihi na nimeingia kwenye vita.
“Nipo tayari kupigana, nina imani kwamba kutakuwa na watu wengine wapo nyuma yangu wengi watanifuata,” alisema.
Wema
aliyekuwa na mama yake mzazi, Miriam Sepetu ambaye naye alitangaza
kuhama CCM na kuhamia Chadema, alisema alipokuwa kada wa CCM alikuwa
mwaminifu na kwa kipindi chote alikipigania kwa uwezo wake wote.
“Nimetuhumiwa
hivi karibuni na nilivyokuwa kama kada nilijitoa maisha yangu, utu
wangu, nilipoteza muda wangu kupigania kile ambacho nilikiamini ni
sahihi lakini siku moja kisinitupe na kinithamini kwa kile
nilichokifanya lakini tofauti na nilivyokuwa natarajia havikutokea.
“Sisemi
kama nilikuwa nafanya ili nije kubebwa kama princess (binti wa mfalme)
ama queen (malkia) kwa sababu Wema ulikuwa unajitoa basi hata ukikosea
usiadhibiwe au ukiwa unatuhumiwa usichukuliwe hatua, hapana,
sijamaanisha hivyo,” alisema.
Alisema baada ya kushutumiwa aliamua kukaa kimya muda mrefu kwa kuwa alikuwa anatafakari alipokosea.
“Nimekaa
kimya muda mrefu si kwamba nimefurahia kilichotokea, nilikuwa bado
natafakari na kutathmini where did I go wrong (wapi nilikuwa nimekosea).
“Ni
kitu gani ambacho nimekosa na kufanyiwa hichi nilichofanyiwa,
nilichogundua ni kitu ambacho najua mwenyewe siwezi kusema nafurahia,” alisema.
Wema
alisema kitendo cha kutuhumiwa bila wahusika kuwa na uhakika na tuhuma
kimemnyong’onyeza na kumvunja moyo kwa kiasi kikubwa.
“Wanasema
wenyewe ‘tenda wema nenda zako usingoje shukrani’, lakini siku ya
mwisho siwezi kuwa mnyonge kwa sababu naamini there is something called
democracy (kuna kitu kinaitwa demokrasia) katika nchi yangu na hicho
ndicho nataka kukipigania,” alisema.
0 comments :
Post a Comment