WAKATI kikosi cha Simba, kesho Jumamosi kikitarajiwa kushuka uwanjani 
kucheza dhidi ya Prisons ya Mbeya katika Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa 
Taifa, Dar es Salaam, nahodha wa Simba, Jonas Mkude ametoa kauli kuhusu 
nidhamu yake.
Mkude amesema kuwa yeye siyo mtovu wa nidhamu kama anavyodaiwa kauli 
ambayo inaweza kupokelewa kwa hisia tofauti na wenzake na mashabiki wa 
soka ambao mara kadhaa wamekuwa wakimlaumu kuwa ni mtovu wa nidhamu.
Kauli hiyo imekuja baada ya taarifa kuwa kuna baadhi ya wachezaji 
wenzake wa Simba wamemuomba kocha mkuu wa timu hiyo, Mcameroon, Joseph 
Omog kumpokonya Mkude unahodha kutokana na nidhamu yake kuwa mbaya.
Mkude hakusafiri na timu yake kwenda Songea kucheza dhidi ya Majimaji na
 inaelezwa kuwa wenzake hawakufurahishwa na kitendo hicho.
“Mimi siyo mtovu wa nidhamu kama inavyodaiwa na sijui ni kwa nini nimekuwa nikiandamwa na tuhuma hizo kila wakati.
“Ninapokuwa sionekani katika timu siyo kwamba ninafanya kusudi ila 
ninakuwa na matatizo na huwa natoa taarifa kwa viongozi wangu ambao 
nawajibika kwao kila siku ambao ni kocha pamoja na meneja, lakini haya 
ambayo yamekuwa yakisemwa kuwa sina nidhamu ninafanya mambo kwa 
kujiamulia siyo kweli.
“Kama kuna jambo lolote baya ambalo nililifanya na halikuwapendeza na 
hiyo ndiyo ikawa sababu ya kusemwa vibaya kila simu basi naomba 
wanisamehe,” alisema Mkude.


0 comments :
Post a Comment