Mvutano wa kisiasa baina ya vijana wa CCM na CHADEMA kuhusu katazo la mikutano ya vyama vya siasa umezidi kukua huku jeshi la polisi likitarajiwa kutoa tamko kuhusu hali hiyo.
Hali hiyo ya jino kwa jino imejitokeza zikiwa zimebakia siku 16 kabla ya kufanyika kwa mkutano mkuu wa CCM July 23, ambao Baraza la Vijana la CHADEMA ( BAVICHA ) limesema litawasaidia polisi kuuzuia.
Tayari
 BAVICHA limetangaza kuandaa vijana 5000 kutoka sehemu mbalimbali nchini
 kwenda kuzuia mkutano huo utakaotumika kumkabidhi Rais John Magufuli 
uenyekiti wa chama hicho.
Jumatatu iliyopita, Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka 
aliionya Bavicha wasiende Dodoma kuzuia mkutano wa CCM kwa kuwa 
watatumia kila mbinu kuwazuia ili kulinda heshima ya chama chao. 
Shaka 
alisema mkutano huo utafanyika kama ulivyopangwa, hivyo Bavicha kama 
kweli ni vidume wa mbegu wajitokeze ili wakione cha mtema kuni. 
Shaka 
alisema UVCCM wako tayari kuidhihirishia dunia kwa kuwatia adabu Bavicha
 na kuonya wasijaribu kufanya jambo lolote linalotishia kuhatarisha 
usalama au ustawi wa maendeleo ya kisiasa ya CCM kwa saa, siku, wakati 
na mahali popote. 
Shaka aliwataka Bavicha kuacha siasa za mikwara, 
vitisho, kutishia usalama na amani ya nchi kwa kujifanya vijogoo wakati 
hawana lolote wanaloweza ama kuzuia, kujenga au kubomoa. 
Alipoulizwa 
kuhusu mvutano huo, Msemaji wa Polisi nchini, Advera Bulimba alisema 
jeshi hilo litatoa taarifa na ufafanuzi kuhusu zuio la mikusanyiko ya 
vyama vya siasa leo. 
Sintofahamu ilivyoanza 
Utata huo uliibuliwa na amri 
ya Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Polisi Makao, Nsato Mssanzya ya 
kuzuia mikutano na maandamano yote ya vyama kwa madai kwamba vyanzo 
vyake vya kiintelejensia vilibaini kuwapo kwa uwezekano wa kutokea kwa 
vurugu. 
“Jeshi la polisi nchini linapiga marufuku maandamano na mikutano
 yote ya hadhara kuanzia Juni 7, mwaka huu hadi hapo hali ya usalama 
itakapotengamaa." Ilisema sehemu ya taarifa ya jeshi la polisi
Baada ya katazo hilo, jeshi hilo lilitawanya mikutano ya ndani ya Chadema, yakiwamo mahafali ya vijana wa chama hicho (Chaso) yaliyopangwa kufanyika Dodoma kwa madai ya kuwapo mlipuko wa ugonjwa usiofahamika.
Baada ya katazo hilo, jeshi hilo lilitawanya mikutano ya ndani ya Chadema, yakiwamo mahafali ya vijana wa chama hicho (Chaso) yaliyopangwa kufanyika Dodoma kwa madai ya kuwapo mlipuko wa ugonjwa usiofahamika.
Hatua hiyo ya polisi ilikuja baada ya 
Chadema kutangaza mpango wa kuzunguka nzima kueleza masaibu ya 
kidemokrasia yanayokikumba na baadaye CCM kutangaza kupita katika maeneo
 hayo ‘kufuta nyayo”.
Katibu wa Bavicha, Julius Mwita alisema mpaka jana
 tayari vijana 5,000 walikuwa wakijiandaa kwenda Dodoma; “kushirikiana 
na polisi kuwafundisha CCM kuheshimu amri zinazotolewa na viongozi. "
"Tumeandaa vijana 5,000 kutoka mikoa 19 nchini ambao wamejitolea kwa 
nauli zao kwenda Dodoma kushirikiana na jeshi la polisi kuhakikisha 
mkutano wa CCM haufanyiki.” 
Watembelea Butiama Katika hatua nyingine, viongozi wa Chadema juzi walitembelea kaburi la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere huko Butiama, wakisema walikwenda kumshtaki Rais Magufuli kwa kuminya demokrasia.
Watembelea Butiama Katika hatua nyingine, viongozi wa Chadema juzi walitembelea kaburi la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere huko Butiama, wakisema walikwenda kumshtaki Rais Magufuli kwa kuminya demokrasia.
Mwenyekiti wa Bavicha, Pastrobas 
Katambi alisema chama hicho kinatambua jitihada zilizofanywa na Mwalimu 
Nyerere katika kukuza na kuendeleza ustawi wa jamii ya kidemokrasia 
nchini.
“Tunapenda kuwaambia watawala kwamba amani ni tunda la haki na ni
 muhimu utawala ukaheshimu misingi ya kikatiba iliyoachwa na Baba wa 
Taifa,” alisema Katambi. 
Kauli za CCM, Chadema 
Naibu Katibu Mkuu 
Chadema, John Mnyika alisema anabariki maandalizi ya mpango na kitendo 
kinachotarajiwa kufanywa na Bavicha ili kuwepo na usawa wa kidemokrasia. 
“Kama ni ruhusa iwe kwa wote na kama zuio liwe kwa wote, haina maana 
Chadema wazuiwe lakini CCM waendelee na mikutano yao ya kisiasa,” 
alisema Mnyika. 
Kaimu Katibu wa CCM, Mkoa wa Dodoma alisema mkutano huo 
ni wa kitaifa na wala si wa mkoa na kushauri atafutwe Msemaji wa CCM, 
Christopher Ole Sendeka. 
“Sisi tunatekeleza maagizo tunayopewa na si 
vinginevyo,” alisema. Ole Sendeka hakupatikana na simu yake ilikuwa 
inaita bila kupokelewa. 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro 
Mambosasa alisema mkutano wa CCM ni wa ndani wala hakuna tatizo lolote 
kwa kuwa mikutano ya ndani inaruhusiwa na kuwa jeshi hilo litawalinda 
wanaCCM. 
Kuhusu Jeshi hilo kuzuia mikutano ya Chadema, Mambosasa alisema
 walizuia bendera na si vinginevyo na kuwa alitoa taarifa ikiwa kamili 
lakini waandishi walipotosha. 
Manyara wajiandaa
Zaidi ya vijana 560 wa 
Mkoa wa Manyara, wamejiandikisha tayari kuelekea Dodoma kwa ajili ya 
kuwasaidia polisi kuzuia mkutano wa CCM ili kuunga mkono agizo la 
kupigwa marufuku mikusanyiko ya kisiasa.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi 
wa Mkoa wa Manyara, Francis Massawe aliwataka vijana hao kuachana na 
mpango huo wa kitoto kwani wao wamejipanga kushughulika na watu 
wanaotaka kuanzisha vurugu. 
Kamanda Massawe alisema endapo kuna kundi 
linataka kukwamisha mkutano halali wa CCM wa kumchagua mwenyekiti wao, 
wasubiri hadi mwaka 2020 ndipo wafanye na kwamba polisi hawatakubali 
hilo litokee. 
“Hao vijana wanacheza ngoma ya kitoto ambayo haikeshi 
kwani wanaingilia majukumu ambayo siyo yao, uchaguzi wa CCM hauna ubishi
 lazima ufanyike na hakuna wa kuzuia, hao wanacheza kombolela,” alisema. 
Msimamo wa Zitto
Akizungumzia uamuzi wa Bavicha, Kiongozi wa ACT 
Wazalendo ambacho pia mitano yake imezuiwa, Zitto Kabwe alisema haoni 
tatizo kuhusu suala hilo kwa kuwa wanafanya siasa, hivyo haoni kama ni 
njia mbaya.
Zitto alisema chama chake hakiwezi kusema moja kwa moja 
kuwa kinaunga mkono uamuzi wa Bavicha lakini wao watakwenda mahakamani 
kupinga hatua ya Serikali kuzuia uhuru wa vyama vya siasa kufanya 
mikutano yao.  



Blogger Comment
Facebook Comment