Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)
imezitaka Michuzi TV, AYO TV na Global TV kusitisha huduma zao za TV
mtandaoni hadi hapo kanuni za usajili rasmi ambazo mamlaka hiyo imesema
inaandaa kwa huduma hizo zitapokuwa tayari.
Barua hiyo, iliyosainiwa na Mkurugenzi
Mkuu Mhandisi James Kilaba tarehe 30 January mwaka huu, imevitaka vyombo
hivyo ambavyo vinapendwa sana nchini na nje ya nchi kuacha mara moja
kutoa huduma za TV mtandaoni.
“Kwa mujibu wa section 13 (1) of
the electronic and postal communications Act Cap 306, sheria za Tanzania
zinahitaji watoa huduma zozote za aina hiyo wanahitaji leseni kutoka
mamlaka ya mawasiliano,” imesema barua hiyo.
Wamiliki wa mitandao hiyo Millard Ayo,
Ankal Issa Michuzi na Abdallah Mrisho wameeleza kushtushwa kwao kwa
agizo hilo la ghafla, tena wakati hata kanuni zenyewe hazijawekwa.
“Global TV ipo tayari hata leo
kukamilisha taratibu za usajili kama zingekuwepo na kwa sababu bado
kukamilika tunaomba kupewa muda zaidi chini ya uangalizi wakati
tunasubiria kanuni hizo mpya,” alisema Abdallah Mrisho, Meneja Mkuu wa Global Publishers.
Ankal Michuzi na Millard Ayo waliunga
mkono kauli hiyo na kwa pamoja watatu hao wameomba kuonana na mkurugenzi
wa TCRA ili kuwasilisha maombi rasmi ya kuruhisiwa kuendelea kutoa
huduma hiyo kwa muda wakati kanuni zikisubiriwa.
Bahati mbaya Mhandisi Kilaba alikuwa safari na swala hilo limepangwa kushughuliwa ataporejea wiki ijayo.
“Ukizingatia kwamba tumekuwa
tunatoa huduma hii kwa muda mrefu na haijulikani kanuni zitakuwa tayari
lini tunaomba TCRA iangalie namna ya kufanya ili wananchi wanaotutegemea
sana wasikose huduma hii,” alisema Ankal. Hata hivyo vituo hivyo vitatu vinaendelea kuhudumu nje ya mchakato wa TV mtandao.
Ayo TV, Michuzi TV na Global TV ambazo
zina watazamaji wengi ndani na nje ya nchi, ni TV mtandao pekee
zilizoitikia mwito wa TCRA kati ya vituo mtandao takriban 51
vilivyopata barua hiyo.


0 comments :
Post a Comment