Vigogo Shirika la Posta Watenguliwa Nafasi zao.....Wengine Wasimamishwa Kazi

Taarifa kamili ya bodi hiyo kama ilivyowasilishwa na Mwenyekiti wake, Dk. Haruni Kondo jijini Dar es Salaam jana.

  ***
Kwa kuzingatia maendeleo ya mageuzi makubwa yanayojitokeza katika sekta ya mawasiliano, Shirika la Posta Tanzania kama mtoa huduma kwa umma (Public Postal Operator), linawajibika kuhakikisha kuwa huduma za kisasa zinazozingatia vigezo vya ubora, usalama, uadilifu katika utendaji na uwajibikaji zinawafikia watu wengi zaidi katika maeneo yote ya nchi.

Kwa hivi sasa Bodi ya Wakurugenzi pamoja na Menejimenti imechukua hatua katika maeneo yafuatayo:-

1) KUPAMBANA NA UHALIFU WA MADAWA YA KULEVYA.
Shirika la Posta Tanzania limechukua hatua kadhaa ili kuhakikisha linashiriki na kuchangia kikamilifu jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano za kupambana na uhalifu, ikiwa ni pamoja na usafirishaji, uuzaji na utumiaji wa madawa ya kulevya, usafirishaji na utakatishaji wa fedha haramu, ugaidi, udanganyifu katika utambulisho pamoja na uhalifu mwingine wa kimtandao wa Kitaifa na Kimataifa.

Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika imedhamiria kuongeza msukumo na kasi ya usimamizi ili kupambana na uhalifu huu ambao una madhara makubwa kwa jamii.

Hatua mojawapo zilizochukuliwa na Shirika ni kusimika mfumo wa kisasa wa kudhibiti usalama na kurahisisha utambuzi wa vitu na matukio hatarishi na haramu yanayopitishwa au kujitokeza kupitia mtandao wa Shirika.

Mfumo huu uliogharimu zaidi ya shilingi milioni mia mbili (200) ambao unajumuisha ufungaji wa kamera za kiusalama (CCTV) katika Posta Kuu ya Dar es Salaam, tayari mzabuni aliyeusimika ameshakamilisha kazi yake na ataukabidhi kwa Shirika wiki ijayo na utazinduliwa rasmi wakati wowote kuanzia hapo.

Aidha, tumesimika mifumo ya kisasa ya kiusalama ikiwa ni pamoja na mashini za ukaguzi wa mizigo (baggage scanners) katika Ofisi zenye uwezekano wa kuwa uchochoro wa uhalifu wa aina hii ikiwa ni pamoja na Ofisi za Zanzibar, Kigoma, Dar es Salaam na Arusha.

Hatua hii imechukuliwa kwa kuzingatia kuwa matukio ya uhalifu uliopangwa (organized crimes) yamekuwa ni changamoto kubwa kwa Mashirika ya Posta Duniani na hivyo tumedhamiria kuhakikisha kuwa, mtandao wa Shirika wa Kitaifa sio uchochoro wa uhalifu huu.

Vitu visivyoruhusiwa kusafirishwa katika mtandao wa Posta kwa mujibu wa sheria ni pamoja na madawa ya kulevya, bidhaa za kemikali zenye sumu, silaha za moto na milipuko, wanyama hai, nyara za Serikali, vifaa vya mionzi, vyakula vinavyooza, betri za aina mbalimbali, vimiminika, fedha haramu, utakatishaji wa fedha na vitu vyovyote hatarishi.

Katazo la vitu hivi kusafirishwa katika mtandao wa Posta limezingatiwa katika sheria na taratibu mbalimbali za Kitaifa ikiwa ni pamoja na sheria ya Mawasiliano ya Elektroniki na Posta (EPOCA) ya mwaka 2010, Umoja wa Posta Duniani (UPU), Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO) na Shirika la Forodha Duniani (WCO).

Kwahiyo, Shirika la Posta Tanzania kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usimamizi wa sheria, kwa hivi sasa limeimarisha uhakiki wa mifumo yake na pia ukaguzi wa barua, vifurushi, vipeto na mizigo ili kujiridhisha juu ya usalama na uzingatiaji wa sheria.

2)   UANZISHWAJI WA JAMII CENTRE
Hatua nyingine iliyochukuliwa ni uanzishwaji wa kituo cha kisasa cha huduma ya Jamii Centre katika Posta Kuu ya Dar es Salaam iliyoko mtaa wa Azikiwe.

Maandalizi ya Ofisi ikiwa ni kaunta za kutolea huduma, mifumo ya mawasiliano, samani kwa wateja, mafunzo ya wahudumu na vifaa vya kazi tayari vimefungwa ili vitumike na kituo kiko tayari kwa uzinduzi, wakati wowote kuanzia sasa.

Kituo kinatoa huduma jumuishi za kimtandao katika sehemu moja (One Stop Community Centre) ili kuwapunguzia wananchi usumbufu wa kufuata huduma hizo maeneo mbalimbali tofauti.

Huduma zinazotolewa kwa njia ya mtandao kwa sasa ni pamoja na:-
Malipo ya wastaafu (NSSF)
Malipo ya gawio (dividends) za makampuni mbalimbali
Malipo ya usajili wa Baraza la Mitihani
Huduma za kibenki- CRDB
Moneygram
Maxmalipo (Road lincense), Luku, Ving’amuzi n.k
Huduma mbalimbali za Posta.
Bodi imeelekeza Menejimenti kuendelea na ushawishi kwa makampuni na taasisi nyingine kama RITA, NHIF, NIDA, Mabenki n.k ili kujiunga na mfumo huu wa kisasa.  Hapo baadae zichukuliwe hatua za kufungua vituo vingine katika miji/mikoa ya Zanzibar, Dodoma, Mbeya, Mwanza, Arusha na Morogoro kabla kufikia mwisho wa 2017.

3)   USIMAMIZI WA KADA ZA UONGOZI NA RASILIMALI WATU
Baada ya Bodi kufanya tathmini yake juu ya utendaji wa Wafanyakazi wa Shirika, imeelekeza Menejimenti ichukue hatua stahiki kwa kada zote za Wafanyakazi kuanzia hapa Makao Makuu, Zanzibar, Mikoani, Wilayani hadi Vijijini.

Bodi inatambua kuwa ufanisi wa Shirika hili utatokana na utendaji wa Rasilimali watu iliyopo. Kwa hivi sasa Shirika lina Wafanyakazi wenye ajira ya kudumu wapatao 1,082 hadi kufikia Disemba 2016 lakini, baadhi yao wanafanya kazi kwa mazoea na lazima sasa wabadilike.

Menejimenti iendelee kusimamia uwajibikaji wa Viongozi na Watumishi wa kada zote ndani ya Shirika ili kujenga nidhamu ya kazi, kujituma, kuheshimu kanuni na taratibu, kuongeza ubunifu na kufanya kazi kwa ufanisi wenye tija kwa Shirika.

Bodi inatambua jitihada za Menejimenti za kuwa na mkakati wa kuimarisha usimamizi na udhibiti wa nidhamu za Wafanyakazi hususani katika kuwaongezea uwezo, kutokana na mafunzo wanayopewa kulingana na uhitaji wa soko, utii, uaminifu na hamasa katika utendaji wa kazi.

Ili kuthibitisha hilo, Wafanyakazi wanapoajiriwa wanakula viapo vya utii na kutunza siri katika utendaji kazi wao na tunapenda kuendelea kuajiri Wafanyakazi wenye uwezo na fuzu sahihi ili kuendana na mabadiliko ya soko na Wafanyakazi waendelee kupewa mafunzo ya mara kwa mara ili kuongeza ufanisi na dhana ya kumjali mteja.

Aidha, kwa wakati huu kuna mwelekeo mzuri kwani Shirika limeanza kuwapima Wafanyakazi kwa kutumia mfumo wazi wa kazi (OPRAS) kwa kuanzia mwaka huu wa fedha 2016/2017, na itakapobainika kuwa wapo Wafanyakazi ambao hawakufikia viwango vya utendaji lazima wawajibishwe.

Kwa kuzingatia yote hayo, katika kikao chake cha jana  tarehe 24/2/2017 Bodi ilipitia kwa makini utendaji, uwajibikaji na nidhamu na uwezo wa watendaji wakuu katika Shirika hilo ambao wanatakiwa kuwa mfano bora wa uongozi wa utendaji mzuri .

Imebainika na kujiridhisha kuwa baadhi ya watendaji wakuu Makao  Makuu ya Posta wamekuwa kikwazo katika dhana ya uwajibikaji, weledi, na kujituma katika kutekeleza wajibu na majukumu yao ili kulifanya Shirika la Posta kuwa mfano bora wa Mashirika yenye ubora katika kutoa huduma.

Aidha, kuna baadhi ya vitendo kwa baadhi ya watendaji vinadhihirisha tabia ya umangimeza, urasimu, kufanya kazi kwa mazoea ubadhirifu na wizi.

Bodi imeamua kufanya mabadiliko ya uongozi wa juu wa Shirika la Posta kwa kutengua nafasi za watendaji wakuu:
1)   Meneja Mkuu Menejimenti ya ya Rasilimali za Shirika Ndg. James M. Sando na kumteua Ndugu Macrice Mbodo kukaimu nafasi hiyo.
2)   Meneja Mkuu uendeshaji wa Biashara Bi. Janeth Msofe na kumteua aliyekuwa Meneja Mkoa Shinyanga Ndugu. Hassan Mwang’ombe.
3)   Imemsimamisha kazi Ndugu. Jasson Kalile aliyekuwa Meneja Msaidizi Mail and Logistic.
4)   Imemsimamisha Kazi Ndugu Ambrose John aliyekuwa Senior Motor Transport Officer.

IMETOLEWA NA:- MWENYEKITI BODI YA WAKURUGENZI SHIRIKA LA POSTA TANZANIA DAR ES SALAAM
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment