Lema Asimulia Mwanzo Mwisho Maisha Ya Gerezani


Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) ameibuka na kueleza mambo mbalimbali, aliyokumbana nayo katika kipindi cha miezi minne akiwa mahabusu katika Gereza la Kisongo mkoani Arusha, kutokana na kukosa dhamana katika kesi ya uchochezi.

Aidha, amesema akiwa katika mahabusu hiyo, alipewa cheo cha nyapara na kuweza kuwaongoza wafungwa wenzake, jambo lililomfanya kufahamu matatizo na manyanyaso mbalimbaliwa, wanayofanyiwa wafungwa.
Lema alisema hayo katika Viwanja vya Ngarenaro jijini Arusha jana, alipokuwa akiwahutubia wakazi wa jimbo lake katika mkutano wa hadhara.
“Kwani nimekosa nini? Kutoa maoni ndio nifanywe hivi kweli? Nilikuwa naomba sana kwa Mungu tangu nilipowekwa ndani hadi siku nilipotoka. 
“Na Mungu aliniambia endelea kuomba na usubiri uone miujiza yangu, lakini akaniambia wasamehe wote waliokukosea kwa kukuweka gerezani bila kosa.”
Akizungumzia kosa alilolifanya la kutoa kauli ya uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli; Lema alisema; “Nilivyosema nimeona maono walidhani mimi ni kichaa, lakini Mungu ndiye atakayethibitisha maono haya, kama yalikuwa ni feki au la.
“Dhambi mbaya na kubwa kuliko zote duniani ni uoga, kinachotesa nchi hii si polisi, ni uoga, angalia kilichotokea juzi mahakamani, nimekaa ndani miezi minne halafu nilipotoka wananchi walikamatwa na kupigwa, kisha wakafunguliwa kesi ya mkusanyiko usio halali, jambo ambalo ni la uonezi,” alisema Mbunge huyo.
Akitoa ushauri kwa polisi, Lema alisema; “ Nawaomba polisi muwe na utu, kwani damu mnayoimwaga itawarudia, hakuna dhambi itakayopandwa ikavuna haki, kwanini mnawapiga watu? Nasema Mungu yupo.”
Alisema Idara ya Mahakama, haipo huru na kwamba kielelezo cha Serikali kuingilia mhimili wa mahakama ni hatua ya hivi karibuni ya Rais Magufuli kumteua Kaimu Jaji Mkuu badala ya Jaji Mkuu.
Alisema lengo la uteuzi huo, aliodai si sahihi, ni kuifanya Serikali icheze na sheria na kwamba tafsiri iliyo ni kuilazimisha Mahakama icheze wimbo wa serikali.
“Hili ni jambo la hatari sana, kwani watu wakijua kuwa Mahakama inayumbishwa na haijasimama imara, haki itatafutwa mitaani. Mateso niliyoyapata Magereza, yamenitengeneza kuwatetea waliopo magerezani.
“Nakuomba Mbunge mwenzangu James Millya (Mbunge wa Simanjiro – Chadema), tukienda bungeni turekebishe sheria, maana tulipozitunga,  tulidhani sisi haitugusi kumbe inatugusa, hivyo tuombe ifanyiwe marekebisho.”
Alisema pia akiwa jela, alishuhudia mambo mbalimbali, ikiwemo kufungwa kwa vijana wadogo wenye umri wa miaka 14 kinyume cha sheria za nchi.
Aliongeza; “Umri huo ni mdogo sana na ninaposema Magereza, lazima mjuwe hali halisi iliyopo magereza.”
Alisema pia alishuhudia kuwekwa mahabusu kwa watu wengine kwa muda mrefu, bila kufikishwa mahakamani au kupewa dhamana, jambo alilosema ni kukiuka sheria za nchi.
Alisema kutokana na uzoefu alioupata mahabusu kwa kipindi cha miezi minne, anaandika kitabu kuhusu wafungwa wanavyoteseka magerezani.
Alisema pia akiwa mahabusu, ameweza kukutana na watu wanaoitwa magaidi zaidi ya 65 wakiwa wamekaa kwa muda mrefu kwa zaidi ya miaka minne; huku wengine wakiwa wamekatwa miguu, lakini cha ajabu ni kuwa hawajahukumiwa kutokana na kutokuwepo kwa ushahidi.
“Unapochelewesha kesi za ugaidi, unajenga tabaka kati ya dini na dini, kama ni magaidi, malizeni upelelezi ili wahukumiwe, lakini kwa upelelezi wangu na uchunguzi wangu sijaona kama hao watu ni magaidi.
“Natoa agizo, mmalize upelelezi kabla sijaenda Bungeni, hii haitakuwa noma ndogo, itakuwa noma kubwa nikienda Bungeni. 
“Kama mimi Mbunge mmeninyima dhamana, kila siku mnaweka mapingamizi narudi gerezani, hali ikoje kwa watu wasioandikwa kwenye magazeti ambao hawajulikani, ni wazi kuwa wananyanyaswa sana,”alisema mbunge huyo.
Kabla ya kuanza kuhutubia, Lema alimpa nafasi msanii, Wema Sepetu ambaye alimtaja kuwa ni mwanamke jasiri na kuwa ana uhakika atashinda katika kesi yake ya kudaiwa kukutwa na dawa ya kulevya.
Akihutubia, Wema alisema ana imani na Mungu na kuwa mitihani ya maisha, anayokumbana nayo ni mipango ya Mungu katika kumfikisha mahali alipo hivi leo.
Alimuomba Lema kusamehe kila analofanyiwa na kutolipiza kisasi ili kupata baraka za mwenyezi Mungu.
Naye, Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Arusha Mjini, Derick Magoma alisema Chadema wilaya Arusha, ipo imara haijayumba wala kutetereka wakati Lema alipowekwa mahabusu kwa kipindi cha miezi minne.
“Hatumpi mtu yoyote kura, bali ni Lema hadi 2020 au zaidi ya hapo, tumefanya maendeleo kwa kipindi cha miaka miwili na wananchi wote mnajua kuwa maendeleo yameletwa na Chadema” alisema.
Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro, alieleza furaha aliyonayo kutokana na kitendo cha kuachiwa kwa Lema. Alisema kwamba miezi minne aliyokaa mahabusu, si jambo la mchezo.
“Mbunge najua walikuweka ndani sababu ya kudhoofisha maendeleo ya Jiji la Arusha, lakini kwa sababu una Meya na madiwani bora wa Baraza la Madiwani, hatukuweza kutetereka” alisema Lazaro.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment