Serikali ya Wilaya ya Same imepiga marufuku biashara ya mahindi ya kuchoma ikiwa ni jitihada za kukabiliana na tatizo la njaa linalokumba maeneo mbalimbali ya nchi.
Agizo Hilo lilitolewa wiki iliyopita na Mkuu wa Wilaya ya Same, Rosemary Senyamile ambapo aliwataka wananchi kuacha biashara ya kuchoma mahindi na kuuza na badala yake wayakaushe na kuhifadhi ili kukabiliana na tishio la njaa.
Alisisitiza kuwa biashara ya uchomaji mahindi kwa sasa ichukuliwe kama jambo lisilo na ulazima (anasa) kutokana na uwepo wa mvua kidogo ambayo imeleta hofu kubwa katika suala la upatikanaji wa chakula nchini.
Licha ya kuwa mvua haijaisha, Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa kuna dalili zote kuwa hakutakuwa na mazao ya kutosha msimu huu, huku akimtaka Afisa Kilimo wa Wilaya kufanyakazi kwa ukaribu na wananchi ili kuhakikisha wanatumia kikamilifu mvua zilizopo.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya amesema kuwa, tishio la njaa katika wilaya hiyo halijaletwa pekee na uhaba wa mvua, kwani majuma kadhaa yaliyopita, ekari 442 za mpunga ziliharibiwa na ndege aina ya quelea quelea katika eneo la Mkomazi.
Chanzo: The Citizen
0 comments :
Post a Comment