WAKATI mshambuliaji Mganda Emmanuel Okwi akitarajiwa kuwasili nchini kesho kwa ajili ya kumalizana na Simba, straika Allan Katerego wa AFC Leopards ya Kenya naye atamwaga wino wa kuitumikia klabu hiyo ya Msimbazi katika msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, imeelezwa.
Taarifa zilizopatikana jana jijini Dar es Salaam, zinaeleza kuwa Okwi atatua nchini baada ya kumaliza majukumu ya kuitumikia timu yake ya Taifa ya Uganda (Cranes) ambayo jana ilikuwa ugenini ikiivaa Cape Verde katika mechi ya Kundi L ya kusaka tiketi ya kushiriki fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 2019.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, tayari mazungumzo kati ya Okwi na viongozi wa Simba yamekamilika kwa asilimia 90 na kilichobaki ni mshambuliaji huyo anaichezea Sports Club Villa kutua nchini kukamilisha mchakato huo.
“Kila kitu kinakwenda vizuri kuhusu Okwi, na makubaliano ambayo yamefikia ni yeye kuja nchini siku yoyote kuanzia kesho baada ya kumaliza mechi ya timu yake ya Taifa, tunaamini hakuna kitakachoharibika kwa upande wake,” alisema kiongozi mmoja wa juu wa Simba.
Mbali na Okwi, Simba inatarajia kumsajili Katerega kwa kumpa mkataba wa miaka miwili. Hata hivyo, mazungumzo kati ya Simba na mshambuliaji huyo wa zamani wa Cranes, yanaendelea vizuri na tayari amekataa kujiunga na mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga ambao nao walimfuata kuzungumza naye baada ya kuonyesha kiwango kizuri katika mechi za michuano ya Kombe la SportPesa inayomalizika jijini leo.
“Naipenda sana Simba, huwa ninafuatilia mechi zao za ligi kupitia Azam TV, ninampenda sana Kichuya (Shiza) anavyocheza, naamini nikipata nafasi ya kusajiliwa mambo yatakuwa poa msimu ujao,” alisema mshambuliaji huyo.
Aliongeza kuwa mkataba wake na AFC Leopards umebakiza miezi sita, lakini anaamini mazungumzo yanayoendelea kupitia meneja wake yatakwenda vizuri naye kuja kucheza katika Ligi Kuu Tanzania Bara. Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ alisema jana kuwa klabu yake itafanya usajili kwa kuzingatia mapendekezo ya benchi la ufundi na itatoa taarifa ya usajili wa mchezaji baada ya kuingia naye mkataba rasmi.Wachezaji wengine wapyaFacebook