Dodoma. Ni dhahiri kuwa mjadala wa hotuba ya bajeti ya mwaka 2017/18 utakaoanza kesho utakuwa mkali mithili ya pilipili kutokana na hisia tofauti zilizojitokeza baada ya Dk Philip Mpango kuuwasilisha bungeni Alhamisi iliyopita.
Wapo wabunge wanaoona hotuba hiyo imegusa wananchi na wapo wanaoona kuwa bajeti imewaongezea mzigo wananchi na hivyo kuna maeneo ya kufanyia kazi ili kutoa unafuu zaidi na kufanikisha ujenzi wa uchumi wa viwanda.
Ikiwa ni bajeti yake ya pili, Serikali ya Awamu ya Tano imependekeza kufuta baadhi ya kodi zilizokuwa kero kwa wananchi wengi na kuahidi kuimarisha ukusanyaji mapato na kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima.
Akiwasilisha bajeti hiyo, Waziri Mpango alishangiliwa kwa nguvu na wabunge wengi waliohudhuria kikao hicho cha Bunge la Saba, hasa alipokuwa akitangaza mapendekezo ya kufuta baadhi ya kodi na ushuru.
Iliyotia fora katika kushangiliwa ni pendelezo ka kufuta kodi ya magari (road license), tozo ya usafirishaji wa mazao pamoja na ushuru wa forodha kwa uingizaji wa mitambo ya uzalishaji na kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika huduma za usafirishaji bidhaa zinazopitia bandari za Tanzania.
Pia, bajeti hiyo iliongeza ushuru katika bia, vinywaji vikali na sigara.
Kadhalika, iliondoa ushuru katika malighafi zinazotumika kutengeneza vifaa vya walemavu.
Ikisubiri kujadiliwa kuanzia kesho, Mbunge wa Iramba Mashariki, Allan Kiula (CCM) alisema yapo maeneo yanahitaji mkazo katika usimamizi wake ili kupata matokeo yaliyokusudiwa.
Alisema mkakati wa kuongeza udhibiti wa usafirishaji madini nje ya nchi kwa kufungua vituo vya ukaguzi, ni mzuri kwa kuwa utaongeza mapato yatokanayo na uzalishaji katika sekta hiyo.
“Bila kujali ubovu wa mikataba iliyopo, suala hili litaongeza tija kwa kuwa tutaweza kudhibiti mapato kwa kiasi kikubwa hivyo Taifa kunufaika zaidi,” alisema.
Kwa sasa kampuni za madini zinalipa mrabaha wa hadi asilimia nne ya thamani ya madini, lakini mapendekezo mapya yanamaanisha wasafirishaji vito hivyo watalipia asilimia moja zaidi katika vituo vya ukaguzi.
Kiula pia alisema sekta ya viwanda itashamiri kwa kuwa kufutwa kwa ushuru wa forodha kwenye mitambo ya uzalishaji ni habari njema kwa wenye viwanda vidogo naa vikubwa.
Alisema kitu muhimu ni kutoweka usumbufu wakati wa kuileta.
Alisema suala hilo pia litakwenda vizuri iwapo kutapatikana mikopo kwa wakulima ili waweze kununua matrekta na kupanua shughuli zao.
Kuna maeneo mawili ambayo Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM) anaitaka Serikali kuyaangalia kabla bajeti haijapitishwa na kuanza kutekelezwa; leseni mpya ya magari na kodi ya mazao.
“Bajeti ni nzuri lakini ina changamoto,” alisema.
Wakati road license na VAT katika usafirishaji wa bidhaa na mizigo nje ya nchi zikifutwa, Serikali imependekeza kupandisha ada ya usajili wa magari kwa Sh50,000 kwa kila aina ya injini ambayo italipiwa mara moja tu wakati wa kusajili gari.
Lusinde anaona katika hilo, wenye magari ya biashara wataongeza nauli kufidia tozo hiyo wakati mwenye magari binafsi watayaegesha.
Suala jingine ambalo Lusinde anataka lifanyiwe marekebisho au mkakati wake uwekwe wazi zaidi ni kufutwa na kupunguzwa kwa tozo za mazao. Serikali imesamehe VAT kwenye vyakula vya mifugo vinavyotengenezwa nchini na kupunguza ushuru wa mazao unaotozwa na halmashauri za wilaya.
Dk Mpango alitaka mabadiliko yafanywe kwenye ushuru huo kutoka asilimia tano zinazotozwa sasa hivi kwenye thamani ya mauzo mpaka asilimia tatu kwa mazao ya biashara na asilimia mbili kwa yale ya chakula huku kodi ya usafirishaji mazao chini ya tani moja ikiondolewa.
“Kufutwa kwa kodi ya mazao kutazinyima halmashauri mapato. Panahitaji marekebisho hapa,” alisema Lusinde.
Mbunge wa Mwanakwerekwe, Ally Salum Hamis haoni dhamira ya dhati ya Serikali kuwapa nafuu wananchi baada ya kuihamishia kodi ya gari katika mafuta.
“Hii si sifa kwa Serikali,” anasema Salum Hamis.
“Kufuta kodi si upendeleo kwa wananchi. Unawezaje kuwatoza kodi nyingi namna hiyo?” alihoji.
Hamis alisema hakuna mkakati wa kujenga uchumi wa viwanda zaidi ya siasa kuingizwa kwenye suala hilo akibainisha umuhimu wa maji kwa mahitaji ya wananchi na viwanda pia lakini kiasi kidogo kimetengwa kwa ajili ya miradi yake.
“Sh13 bilioni zimetengwa kwa ajili ya maji, lakini Sh229 bilioni zitaelekezwa kuimarisha (Shirika la Ndege) ATCL. Viwanda vitaendeshwaje bila maji ya uhakika?” alihoji mbunge huyo.
Mbunge wa Korogwe Mjini, Mary Chatanda alisema bajeti imelenga kutoa unafuu kwa wananchi baada ya kuondoa kodi ambazo zilikuwa kero.
Alisema wamiliki wa nyumba za kulala wageni na hoteli pamoja na wamiliki wa magari sasa wamepata unafuu.
“Wapo waliokuwa wanauza magari yao kutokana kodi hizi,” alisema.
Alipongeza mkakati wa kuboresha miundombinu hasa barabara akisema itakarahisisha usafirishaji wa mazao.