Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa mara nyingine inawakaribisha wadau wake wote kuja kupata huduma mbalimbali katika maeneo ya Utoaji mikopo na Urejeshaji mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu kuanzia leo tarehe 28 Juni hadi tarehe 08 Julai, 2017 katika Uwanja wa Maonesho ya Biashara wa Kimataifa wa J.K. Nyerere (Sabasaba), uliopo Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
Katika kipindi hiki chote; Bodi ya Mikopo itatoa huduma kwa wateja katika banda lake lililomo katika banda kuu la Benjamín William Mkapa kuanzia saa 3.00 asubuhi hadi saa 11.00 jioni. Wadau watajibiwa maswali na kupewa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya Utoaji Mikopo hususan kwa Mwaka wa masomo 2016/2017 na maandalizi ya mwaka mpya wa masomo 2017/2018.
Kuhusu Urejeshaji wa Mikopo; Taarifa za kiasi cha mkopo anaodaiwa mnufaika zitatolewa ambapo Wanufaika ambao hawajaanza kurejesha mikopo yao wataweza kujaza fomu za maulizo (inquiry forms) kwa kutoa taarifa zao za sasa ili Bodi iweze kuanza kukusanya mikopo kutoka kwao.
Kwa upande wa Utoaji mikopo; wadau watapata fursa ya kujua vigezo vinavyotumiwa, utaratibu wa kuomba hadi kupangiwa mikopo, viwango vya mikopo vinavyopangwa; utaratibu wa kukata rufaa na iwapo kuna tatizo la utoaji mikopo kutokana na kutokamilika kwa baadhi ya taarifa za mwombaji mkopo.
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu pia imeandaa machapisho yenye taarifa za utoaji na urejeshwaji mikopo ili kuwagawia wadau watakaotembelea banda lake.
Imetolewa na:
MKURUGENZI MTENDAJI
BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU
Tarehe 28 Juni, 2017