WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angela Kairuki, amesema rufaa za watumishi wa umma wanaopinga kutajwa katika orodha ya wenye vyeti feki zinaendelea kuhakikiwa kwa umakini mkubwa ili haki itendeke.
Kauli ya Kairuki imekuja baada ya hivi karibuni Katibu Mkuu wake, Dk. Laurean Ndumbaro, kulieleza MTANZANIA Jumamosi sababu zilizochelewesha ripoti mpya ya wenye vyeti feki kuwa ni pamoja na uhakiki wa rufaa hizo zilizokatwa kupitia Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) ili kuhakikisha kasoro iliyojitokeza katika ripoti ya kwanza iliyotolewa Aprili 28, mwaka huu isijirudie.
Ndumbaro alisema uhakiki huo kwa sasa upo katika hatua za kuthibitisha watumishi waliokutwa na vyeti visivyokamilika ili kuepuka kuwaweka wengine kimakosa.
Akizungumza mjini hapa jana katika semina ya wabunge wanachama wa Mtandao wa Wabunge wa Kupambana na Rushwa Afrika (APNAC), Kairuki alishindwa kusema ni lini uhakiki huo unaowahusu baadhi ya watumishi kati ya 9,932 waliotajwa kuwa na vyeti feki katika ripoti ya kwanza utamalizika.
Pia alisema Serikali ilifanikiwa kuwaondoa watumishi hewa zaidi ya 10,000 na mchakato huo ni endelevu. “Tumepokea fedha zilizookolewa ambazo ni shilingi bilioni 1.2 kutokana na watumishi hewa zilizokuwa zinarejeshwa katika akaunti maalumu kupitia Takukuru.
“Rushwa imeathiri uchumi na juhudi za Serikali, hatutavumilia kuona rushwa inashamiri, tutapambana bila kujali dhamana aliyokuwa nayo mtu,” alisema.
Alisema hatua mbalimbali zinachukuliwa dhidi ya viongozi wanaojihusisha na rushwa, kwa kuwaondoa madarakani na kuwafikisha mahakamani.
“Utaratibu wa kuamini kwamba ili kupata haki lazima utoe rushwa ukome,” alisema. Akifungua semina hiyo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema Serikali imefanikiwa kuokoa jumla ya Sh bilioni 53.9 kutokana na uchunguzi na operesheni mbalimbali zilizofanywa na Takukuru katika kupambana na vitendo vya rushwa.
“Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuimarisha Takukuru, kuimarisha matumizi ya mashine za kielektroniki, kuanzisha mahakama ya mafisadi, kusimamia nidhamu katika utumishi wa umma na kuchukua hatua za haraka za kinidhamu na za kisheria dhidi ya watuhumiwa wote wa rushwa na ufisadi.
“Tumeanza kupata mrejesho mzuri, watumishi wa umma wanawajibika ipasavyo na vitendo vya rushwa vinaendelea kupungua, kutokana na jitihada zetu hizo, mwaka 2016/2017 Serikali imefanikiwa kuokoa jumla ya shilingi bilioni 53.9 kutokana na uchunguzi na operesheni mbalimbali
zilizochukuliwa na Takukuru,” alisema.
Majaliwa alisema kiasi hicho ni kikubwa ikilinganishwa na Sh bilioni saba zilizookolewa mwaka 2015/2016. Alisema Serikali haina mzaha katika mapambano hayo na aliwaomba wabunge waendelee kuunga mkono, waende kutoa wito kwa wananchi ili nao waunge mkono jitihada hizo za kupambana na rushwa.
“Tumefanya tathmini kubaini mianya ya rushwa katika sekta za ardhi, uchukuzi, biashara na maji, hivyo kuziba mianya hiyo. Tutaendelea kuiwezesha Takukuru ili iendelee kubaini mianya ya rushwa na kutoa ushauri wa kuziba,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa APNAC, George Mkuchika, alisema mtandao huo una jumla ya wabunge 148 na wanatarajia ifikapo mwaka 2019 wafikie robo tatu ya wabunge wote.
CHANZO GAZETI LA  MTANZANIA