Waziri wa TAMISEMI, George Simbachawene
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI), George Simbachawene ametoa onyo kwa wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya wanaoitumia vibaya sheria ya tawala za mikoa inayowapa mamlaka ya kuwakamata na kuwaweka watu ndani kwa saa 48.
Simbachawene ametoa onyo hilo leo, Ijumaa bungeni Mjini Dodoma wakati akitolea ufafanuzi majibu ya swali la mbunge viti maalum, Cecilia Pareso kuhusu wakuu wa mikoa na wilaya wanaoamuru kukamatwa na kuwekwa ndani kwa watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa vijiji bila sababu za msingi.
Simbachawene amesema ni kweli sheria hiyo inawapa mamlaka hayo, lakini hawapaswi kuitumia vibaya kwa lengo la kujionyesha, bali wanapaswa kuwa na uhakika kuwa muhusika amefanya jinai, au anahatarisha amani ya eneo husika kabla ya uamuzi huo.
“Asikamatwe mtu kwa ajii ya show, akamatwe mtu kama kweli amethibitika kuhatarisha amani, sheria hiyo siyo kwa ajili kuonyesha kuwa una madaraka” amesisitiza Simbachawene.
Aidha, kuhusu sheria hiyo kufanyiwa marekebisho kutokana na kutumiwa vibaya, Naibu Waziri wa TAMISEMI, Selemani Jafo amesema kwa sasa sheria hiyo inajitosheleza na haihitaji marekebisho yoyote kwa kuwa ipo kwa ajili ya kuhakikisha amani na usalama vinakuwepo katika wilaya au mkoa husika, na wenye jukumu la kulisimamia hilo ni wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa.Facebook