Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Sahara Media Group Limited (SMGL), Dk Anthony Diallo amewataka watendaji na wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuacha ukaidi dhidi ya walipakodi wanapotekeleza majukumu yao.
Akizungumza kwa njia ya simu akiwa wilayani Ukerewe kwenye ziara ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Rodrick Mpogolo anayetembelea Mkoa wa Mwanza, Dk Diallo alisema TRA na walipakodi ni wabia wanaopaswa kushirikiana.
Dk Diallo ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, alisema TRA inapaswa kutumia njia ya majadiliano katika madai kati yao na walipa kodi, hasa kwa wawekezaji wa ndani kwa sababu wa nje wanaotaka kuja kuwekeza nchini hufuatilia na kuangalia namna wa ndani wanavyofanyiwa.
Mbunge na waziri huyo wa zamani, alikuwa akizungumzia hatua ya TRA kuzifunga ofisi za SMGL inayomiliki vituo vya Redio Free Africa (RFA), Kiss FM na Runinga ya Star Tv kutokana na madai ya kodi yanayofikia Sh4.5 bilioni. “Siwalaumu TRA; hawana makosa kwa sababu wanatekeleza majukumu yao ya kisheria,” alisema Dk Diallo.
Akizungumzia fedha zinazodaiwa na TRA, alikiri kuwa hati ya madai inaonyesha wanadaiwa Sh4.5 bilioni, lakini alisema kuna majadiliano yanaendelea kati ya kampuni yake na TRA kuhusu kiwango halisi.
“Katika deni hilo kuna fedha za VAT tulizokusanya kutoka kwa wateja na kuziwasilisha TRA, pia iko asilimia 30 ya riba inayotokana na ucheleweshaji ambayo tumeomba iondolewa,” alisema.
Dk Diallo alifafanua kuwa majadiliano yanaendelea ili kurejesha huduma zilizofungwa tangu jana mchana.
SMGL yalipa Sh60 milioni
“Tunaendelea kulipa; hata leo (jana) wakati wanatufungia ofisi tulikuwa tumelipa Sh60 milioni. Siamini kama watatufungia milele kwa sababu uwezo wetu wa kulipa deni hilo unategemea sisi kufanya biashara,” alisema Dk Diallo.
Alisema kitendo hicho kimewaathiri wafanyakazi, familia, wateja wa matangazo pamoja na umma unaotegemea kupata habari kupitia vituo vya redio na runinga vilivyofungwa. Katika tukio hilo, wafanyakazi wa sahara waliokutwa ofisini wakati wa kufunga ofisi hizo, kazi iliyotekelezwa na Kampuni ya Suka Security, Court Broker and Auction Mart Limited, walitolewa ndani chini ya ulinzi wa askari.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Liasuka Swalehe alisema deni hilo lisipolipwa ndani ya siku 14, mali za SMGL zitakamatwa na kupigwa mnada.



0 comments :
Post a Comment