Kesi inayowakabili Rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva na Makamu wake, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, imeahirishwa hadi Julai 20, mwaka huu na watuhumiwa hao wamerudishwa rumande.
Kesi hiyo ilikuwa ikitajwa tena leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Victoria Nongwa baada ya watuhumiwa hao kusomewa mashtaka yao kwa mara ya kwanza Juni 29, mwaka huu.
Viongozi hao wanakabiliwa na makosa matano wanayodaiwa kuyafanya kwa nyakati tofauti yakiwemo ya utakatishaji fedha ambayo hayana dhamana.
Miongoni mwa mashtaka yanayowakabili ni pamoja na kughushi nyaraka zinazodaiwa kuwa klabu ya Simba inawalipa madeni watuhumiwa hao kiasi cha dola za Kimarekani 300,000 (Zaidi ya shilingi milioni 700 za kitanzania).
Makosa mengine ni Aveva kutoa nyaraka za uongo kwa Benki ya CRDB Tawi la Azikiwe Dar es Salaam Machi 10, 2016, la tatu ni kutakatisha fedha kinyume cha sheria, ambapo inadaiwa rais huyo na Kaburu walikula njama za kufanya uhalifu huo.


0 comments :
Post a Comment