Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani Geita, kimewavua uanachama na wadhifa vigogo wawili huku kikitoa onyo kwa wanachama wengine kwa kuhusishwa na tuhuma za usaliti na vitendo vya hujuma.
Vigogo hao ni Katibu mwenezi wa Jimbo la Geita mjini, Edward John Manyika pamoja na mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, ambaye pia aligombea udiwani kata ya Kalangalala, Daudi Sunzu Ntinonu.
Katibu wa chama hicho Jimbo la Geita Kangeta Ismail, ametanabaisha kuwa kuonekana kwa vigogo hao wakiwa wamevalia sare za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye mkutano wa kukabidhi nyumba 50 za watumishi wa afya, uliofanyika Julai 10, wilayani Chato na kuhudhuriwa na Rais John Magufuli ni moja ya sababu za kutimuliwa kwa viongozi hao.
Kwa mujibu wa taarifa ya mwandishi wa Azam TV, Ester Sumira aliyopo mkoani Geita, hatua hiyo imefikiwa baada ya kufanyika kikao cha kamati tendaji ya jimbo hilo na kubaini uwepo wa vitendo vya usaliti.
Baada ya kuchukuliwa hatua hiyo, wahanga hao wamekilalamikia chama hicho kutofuata kauli mbiu yake ya “Chama cha Demokrasia na Maendeleo” na kudai kutokuwepo kwa hiyo demokrasia inayotajwa na ndiyo maana wameamua kumuunga mkono rais Magufuli kwa kazi nzuri anayofanya.
Mkutano huo unaotajwa kuwachongea wanachama hao, ulimuhusisha rais mstaafu wa awamu ya tatu Benjamini Mkapa, ambaye alikuwa mgeni rasmi, huku rais Magufuli akiwa mgeni mualikwa.


0 comments :
Post a Comment