POLISI mkoani Mwanza inamshikilia Emmanuel William (21), mkazi wa Mtaa wa Sandula wilayani Magu kwa tuhuma za kujifanya daktari wa Hospitali ya Wilaya ya Magu na kuwatapeli wagonjwa kwa kuwaomba fedha ili awapatie matibabu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema jana kuwa mtuhumiwa alikamatwa Julai 2, mwaka huu saa tatu usiku katika eneo la hospitali hiyo baada ya kuingia kwenye wodi ya wanaume akiwa amevalia suruali nyeupe na glovu.
“Aliingia katika wodi hiyo ya wanaume na kujitambulisha kwa wagonjwa kuwa yeye ni daktari wa zamu na baada ya kujitambulisha alimfuata mgonjwa mmoja jina tumelihifadhi, aliyelazwa wodini hapo na kumuomba shilingi laki moja ili amfanyie mpango apelekwe Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa ajili ya matibabu zaidi,” alisema Kamanda Msangi.
Alisema baada ya kumueleza mgonjwa huyo alimkubalia na kumuomba mtuhumiwa huyo wakutane kesho yake ili aongee na ndugu zake ili wamtafutie kiasi hicho cha fedha alichokiomba na suala la kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa ajili ya matibabu.F