Madiwani 19 wa CUF wa Manispaa za Mkoa wa Dar es Salaam wamempinga Profesa Ibrahim Lipumba na kutangaza kuunga mkono maamuzi ya viongozi wa chama hicho ya kufungua kesi dhidi ya Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa madai ya wakala huo kusajili majina mapya ya wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ya CUF pasipo kujiridhisha juu ya uhalali wa majina hayo.
Msimao wa madiwani hao umekuja siku moja baada ya Profesa Lipumba ambaye ni Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kudai kwamba hakuna chombo chenye uhalali wa kuishitaki RITA mahakani kwani chama hicho hakikuwa na bodi halali tangu Agosti 2015.
Wakati akitangaza maazimio ya madiwani hao leo Julai 5, 2017, Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Mussa Kafana amesema wanapinga juhudi zinazofanywa na Lipumba na wafuasi wake kwa madai kuwa zinalenga kuharibu taswira ya chama hicho kwa jamii na uvunjifu wa amani.
“Sisi Madiwani wa CUF tunaunga mkono hotuba iliyotolewa na Katibu Mkuu Maalim Seif pamoja na maamuzi ya viongozi kupinga maamuzi ya RITA mahakamani ambayo yamekiuka sheria ya wadhamini kifungu cha 26,” amesema.
Pia, Kafana amesema wanaunga mkono pendekezo la chama hicho kuwasilisha mambo katika Mahakama Kuu ya kuitaka isimamishe kesi nyingine za CUF zilizofunguliwa hadi shauri linalohusu uhalali wa maamuzi ya RITA litakapoamuliwa.
Naye Naibu Meya wa Ilala, Omary Kumbilamoto amesema hakuna diwani miongoni mwao atakayekubali kuhojiwa na Kamati ya Maadili na Nidhamu ya Lipumba.
Kwa upande wa Naibu Meya wa Ubungo, Omary Thabiti amesema kuwa CUF ni moja na kwamba hawatambui vyombo vya maamuzi vya Lipumba ikiwemo Bodi ya Wadhamini na Kamati ya Maadili na Nidhamu, na kwamba wamejitoa kukipigania chama hicho.