Timu ya Everton itatua nchini kesho asubuhi tayari kukabili Gor Mahia ya Kenya katika mchezo wa kirafiki wa Sportpesa utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Baada ya kuwasili timu hiyo mchana itafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Taifa, lakini hautaruhusu mtu yoyote kutazama mazoezi yao.
Afisa usalama viwanjani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), Hashim Abdallah aliwataka mashabiki wa soka kutii agizo la timu hiyo kwa kutulia nyumbani na kusubiri siku ya mchezo.
"Everton wameshatoa maelekezo kuwa mazoezi yao hawataruhusu mtu yoyote kuangalia hivyo mashabiki wa soka wanapaswa kutii hilo ili wasiingie katika vita na jeshi la Polisi.
"Pia mashabiki wanatakiwa kununua tiketi mapema ambazo zimeanza kuuzwa leo kupitia Selcom ili kuepuesha msongamano na vurugu siku ya mchezo maana mashabiki wengi wanapenda kununua tiketi siku ya mwisho wakati walikuwa wana muda wa kununu mapema"alisema Hashim.
Hashim alisema wamejiandaa kuimarisha usalama tangu kuwasili kwa timu hiyo mpaka siku ya mechi na watahakikisha siku hiyo barabara za Kilwa na Mandela zinapitika kirahisi ili kuwafanya mashabiki kuwahi uwanjani na kuondokana na foleni.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo, Yusuph Singo alisema Serikali wamehakiksiha uwanja unakuwa katika hali nzuri kwa ajili ya mchezo huo huku mgeni rasmi katika mchezo huo akiwa ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu.
Mkurugenzi wa Utawala na Utekelezaji wa kampuni ya Sportpesa, Abbas Tarimba alisema leo mchezaji wa zamani wa Everton , Leon Osman ataendesha semina ya uongozi kwa viongozi wa klabu nchini na itafanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Julai 12."



0 comments :
Post a Comment