Nikishauri sasa watumiwe kumaliza mgogoro wa mauji ya polisi na raia Kibiti na Mkuranga, mkoani Pwani.
Wasifu wa viongozi hawa wa polisi, kama aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Wolfgang Gumbu, upo kwenye historia ya taifa hili.
Gumbu alitokomeza uhalifu Dodoma kipindi chake na kupongezwa na wengi leo hii atashindwa nini kusaidia kupatikana kwa ufumbuzi wa tatizo la Kibiti?
Kahama mkoani Shinyanga kulitisha kwa uvamizi na uporaji kwenye nyumba za wageni. Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga Abdallah Mssika, alitokomeza tatizo hilo, akishirikiana na Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Simon Sirro, wakati huo akiwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa.
Leo Afande Mssika hana cha kushauri kuhusu mambo ya Kibiti kweli?
Usipokubaliana nami, chukua muda kujihoji vichwa vya nguvu kama cha Alfred Tibaigana , Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam, ambaye kabla aliwahi kuongoza operesheni za kusaka na kuangamiza kundi la wauaji ndani ya pori la Ngorongoro, anasahaulikaje Kibiti?
Kuna wengine wengi leo tunajiuliza vichwa hivi vinatumikaje kwa maendeleo ya Tanzania? Havitumiki kwa vyovyote kwa sababu wenye vichwa hivyo wanachukuliwa kuwa 'ni polisi tu’, acheni kuwapuuza ni hazina kubwa.
Inawezekana wataalam hawa wanaombwa ushauri lakini hiyo si rasmi. Hebu waingizwe kwenye ushiriki rasmi kwa maslahi ya nchi. Serikali na itafakari.
Ni ukweli kuwa mauaji ya mfululizo ya Kibiti na Mkuranga mkoani Pwani ni suala zito linaloliumiza taifa, kuanzia familia za walioathirika, taasisi za usalama na kila mmoja ambaye anathamini utu wa mtu na haki ya maisha ya kila binadamu.
Ukubwa wa tatizo hili unatulazimisha tujenge ushirikiano wa nguvu wa kitaifa wa kulimaliza. Kwa hali ilivyo, ni vigumu kwa jeshi la polisi pekee kulimaliza tatizo hilo bila kuhusisha wadau na wabobezi wakiwamo vigogo wastaafu.
Ninaona vichwa vya wabobevu kama Wakuu wa Jeshi la Polisi wastaafu Omar Mahita na Said Mwema, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Adadi Rajab, lakini pia Kamanda mstaafu Tibaigana miongoni mwa wengine wengi walioondoka ndani ya jeshi hilo katika vyeo tofauti.
Watanzania hao ni miongoni mwa wengi wenye akili na utimamu katika uongozi na ulinzi, maoni thabiti, mipangilio ya nguvu na mikakati ya kisayansi ya kukabili matukio ya kihalifu.
Baadhi wakiwa wamepata mafunzo ya kiweledi ndani na nje ya nchi, wametapakaa Tanzania nzima baadhi wakifanya shughuli binafsi, wengine kwenye idara za umma, binafsi na hata za kimataifa huku baadhi wakiwa kwenye miradi ya wawekezaji.
Kuna polisi wengine kadhaa , baadhi walikuwa wakuu wa vituo, wakuu wa upelelezi wilaya, wakuu wa polisi wilaya, wakuu wa upelelezi mikoa na makamanda wa polisi wa mikoa iwe Bara na Visiwani.
Vichwa hivyo vikitumika kikamilifu, tatizo la Kibiti litamalizika pengine kwa urahisi. Nimeeleza ni vigumu askari waliopo kazini kulimaliza wenyewe kwa sababu hakuna mtu wa eneo la mauaji aliye tayari kushirikiana na polisi akiogopa naye kuingizwa kwenye orodha ya watu wanaolengwa kuuawa.
Hata askari wenyewe ni walengwa kwenye mauaji hayo. Pengine ni rahisi kwa askari wastaafu ambao sasa ni raia wenye utaalam wa upelelezi kupata taarifa kamili na za uhakika za matukio hayo.
Tatizo la jamii yetu ni dharau ya wazi kwa mtu aliyekuwa afisa wa polisi. Hata maafisa wa polisi wenye elimu ya udaktari wa falsafa, hudharauliwa! Kwa bahati mbaya dhana hiyo huanzia ndani ya jeshi lenyewe mpaka nje.
Haishangazi maafisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wakipewa nyadhifa za kisiasa kama ukuu wa mikoa lakini afisa mmoja mstaafu wa Jeshi la Polisi akipewa wadhifa huo, huonekana ajabu hata kama ana elimu kubwa na uwezo, weledi na ni mchapa kazi.
Mtu kutoka polisi anayeajiriwa kwenye taasisi ya umma akiwa mwanasheria na wakili wa mahakama, mhasibu, daktari, mtaalam wa rasilimali watu na utawala na taaluma nyingine huchukuliwa kuwa ‘polisi tu’ bila kuzingatiwa taaluma yake! Pamoja na uwezo wake na utaalaam mwingi alionao kichwani, atabakishwa kuwa chini tu akiponzwa na upolisi aliopitia!
Jeshi la Polisi likitoka kwenye mawazo hayo potofu dhidi ya wataalam waliopitia na kulitumikia , mauaji ya Kibiti yatapata ufumbuzi.
Cha kufanya ni kusajiliwa rasmi kwa maofisa wastaafu wa polisi popote walipo Tanzania na kuona jinsi wanavyoweza kutumika kwanza kutafuta sababu za mauaji ya Kibiti na pili kuubaini mtandao mzima wa wauaji.
0 comments :
Post a Comment