Makamu wa rais , Samia Suluhu Hassan amesema taifa halipo tayari hata kidogo kupokea misaada yenye masharti ambayo yanakiuka mila na desturi za nchi.
Kauli ya kiungozi huyo ameitoa leo Ijumaa, Julai 14, baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na rais mstaafu wa Ireland, Mary Robinson pamoja na mwanzilishi wa Taasisi ya Graca Machel, Craca Machel Ikulu jijini Dar es Salaam.
Makamu wa rais ametanabaisha uwepo wa baadhi ya wafadhili wanaisaidia serikali vizuri katika kutekeleza miradi ya maendeleo na bajeti bila masharti mabaya, na kuelezea uwepo wa baadhi ya wafadhili wanaoonesha wazi kutaka serikali ikubali masharti yao ambayo yanaenda kinyume na maadili ya taifa.
Mama Samia amepinga vikali jambo hilo na kuongeza kuwa kutokana na changamoto hiyo, serikali itaendelea kusimamia maadili ya taifa ipasavyo huku ikiweka mikakati mizuri kwa ajili ya kuongeza mapato yake ya ndani na hatimae kuondokana na utegemezi.
Miongoni mwa mambo ambayo nchi nyingi za Afrika zimekuwa zikikabiliana nayo kutoka kwa baadhi ya mataifa yaliyoendelea kiuchumi huku yakiambatana na masharti magumu, pamoja na kuwepo kwa shinikizo la kukubali ndoa za jinsia moja na mikopo yenye riba kubwa.