Emmanuel Okwi akisaini mkataba rasmi kuichezea klabu ya Simba.
Mshambuliaji mpya wa Simba Emmanuel Okwi amepewa onyo kali na beki wa Yanga kuwa hakuna masihara ligi Kuu, ajipange
Kuelekea msimu mpya huku usajili ukiendelea kufanyika, beki mahiri wa Yanga Nadir Haroub ‘Cannavaro’ amemuonya mshambuliaji mpya wa Simba, Emmanuel Okwi kwa kumwambia asitarajie mteremko katika msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.
Kwa mujibu wa gazeti la Championi, Cannavaro ameyasema hayo baada ya Simba kumrudisha Okwi katika kikosi chake akiwa amewahi kuitumikia timu hiyo kwa vipindi viwili tofauti, pia akiwa amewahi kuichezea Yanga sambamba na beki huyo
Cannavaro amesema anajua Okwi ni mchezaji mzuri ambaye anaijua vizuri ligi kuu, lakini hapaswi kuichukulia kama alivyoiacha kutokana na ushindani kuongezeka.
“Okwi amerudi Simba, ni kitu kizuri kwa ajili ya kuitengeneza timu yao ambayo ni washiriki wa michuano ya kimataifa msimu ujao, Okwi ni mchezaji mzuri, nimecheza naye timu moja lakini pia alikuwa mpinzani.
“Asitarajie mteremko kwani mambo yamebadilika sana, yeye alienda kucheza Ulaya, sasa amerudi lakini ni vyema akajua kuwa ligi ya hapa kwa sasa imebadilika ushindani umekuwa mkubwa.
“Angalia msimu uliopita jinsi bingwa alivyopatikana hapo ndiyo utaelewa, wakati ule alikuwa hana mwili mkubwa sijui sasa yupoje kwani kila kitu kinabadilika kutokana na wakati,” alisema Cannavaro.