Mbunge wa Singida Mashariki ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Lissu leo amegoma kutoka katika chumba cha mahakama kufuatia kuwepo kwa tetesi kuwa kuna baadhi ya polisi wametumwa kumkamata kiongozi huyo.
Tundu Lissu ambaye yupo mkoani Dodoma kuwatetea wateja wake katika kesi mbalimbali amesema kuwa amepata taarifa kuwa wapo baadhi ya polisi wametumwa kumkamata hivyo ameamua kubaki katika chumba cha mahakama ili hao polisi waingie kumkamata akiwa mahakamani hapo.
“Waje wamkamate Rais wa Chama Cha Mawakili wa Tanganyika ndani ya mahakama alipokuwa anafanyia kazi halafu wafanye hayo waliokuwa wamezoea kuyafanya, tatizo siyo kukamatwa na kukaa saa 48 bali tatizo tunakamatwa kwa kutekeleza wajibu wetu kama raia wa nchi yenye katiba inayotambua haki za binadamu, tunakamatwa kwa kuisema serikali vibaya, tunakamatwa kwa sababu ya kutenda haki yetu ya kutoa maoni” alisema Tundu Lissu
Hivi karibuni Tundu Lissu alitoa kauli dhidi ya serikali ya awamu ya tano pamoja na Rais na jana kupitia msemaji wa serikali Dkt. Hassan Abbasi serikali ilitoa kauli dhidi ya Tundu Lissu na kumtaka kuacha propaganda.
Baada ya muda Polisi Waamua kumfuata ndani ya Mahakama.
RPC wa Dodoma amemfuata Tundu Lissu ndani ya Mahakama na kumuambia kwamba hajaagiza mtu yoyote kumkamata, hivyo asiogope kutoka nje. Amemwambia atoke tu kwani hajapata maagizo yoyote ya kumkamata Lissu. Sasa Lissu Kashatoka Mahakamani yupo Nyumbani kwake Area D. “Uwe na amani, hakuna atakaye kusumbua”. Amesema RPC wa Dodoma.


0 comments :
Post a Comment