Sakata la vyeti feki limewakosesha huduma za afya baadhi ya wananchi, huku waganga wa mikoa wakilia na Serikali wakitakaiajiri haraka watumishi wa kada hiyo 7,304 vinginevyo hali itakuwa mbaya.
Mwenyekiti wa waganga wa mikoa, Dk Leonard Subi jana alimweleza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, George Simbachawene kuwa hali ni mbaya kwa zahanati na vituo vya afya.
Dk Subi amesema vyeti feki viliondoka na watumishi 3,439 na kufanya upungufu wa watumishi katika kada hiyo kufikia asilimia 49.5 ambayo ni sawa na nusu ya watumishi wanaohitajika.
“Mheshimiwa waziri, jumla ya zahanati 285 hazina mtumishi mwenye ujuzi hata mmoja, hivyo zinaongozwa na wahudumu wa afya huku vituo vya huduma 1,505 vikikosa kabisa waganga CO au CA navyo vinaongozwa na wauguzi ambao kimsingi kazi yao ni uuguzi tu,” amesema Dk Subi.
Waziri Simbachawene alikiri kuwa bado huduma ya afya nchini hairidhishi lakini Serikali inaliangalia suala hilo kwa umuhimu wake, ikiwamo kuwabaini wasiokuwa na tija katika nafasi zao ili wawapishe wenye uwezo.
Simbachawene amesema Tanzania haijafikia lengo linalotarajiwa jambo ambalo linazidisha uchungu kwa wananchi kwa kuwa afya ndiyo kila kitu kwa maisha ya mwanadamu.
0 comments :
Post a Comment