Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe amesema, kupona kwa mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ni mpango wa Mungu na kwamba wataendelea kutoa taarifa za maendeleo yake kwa kadiri wauguzi na madaktari watakavyowafahamisha.
Kiongozi huyo wa Chama kikuu cha Upinzani, Chadema amesema hayo kufuatia mahojiano yake na moja ya chombo nchini, baada ya kutakiwa kueleza hali ya kiongozi huyo pia wa mawakili ambapo amedai kuwa kwa sasa hawawezi kusema chochote kilicho nje ya hali ya mgonjwa.
“Maendeleo ya Lissu tunayatoa kulingana na madaktari wanavyotuambia, hatuwezi kusema chochote nje ya wataalam hao, kwa kuwa wao ndiyo wenye ujuzi wa kumtibu na kujua maendeleo yake, ingawa sisi wote tuna hamu apone mara moja aje aendelee kupigania haki za wanyonge kama alivyokuwa akifanya,” alisema Mbowe
Kiongozi huyo amewataka Watanzania wazidi kumuombea Tundu Lissu na kuendelea kuchangia gharama za matibabu kwa kiongozi huyo kwani matibabu yake ni ghali mno na kama chama peke yao hawatoweza.
“Watanzania wenzetu waendelee kumuombea kwa Mungu pamoja na kuchangia gharama za matibabu, kwa kuwa gharama zake ni kubwa ambazo chama pekee hakiwezi kuzimudu bila ya misaada kutoka kwa watu mbalimbali”alisisitiza Freeman Mbowe.
Lissu yupo mjini Nairobi, Kenya katika matibabu kufuatia kupigwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 7, mwaka huu akiwa mjini Dodoma na baadaye kusafirishwa na kwenda nchini humo kwa matibabu.