Emmanuel Okwi ameendelea kuwa gumzo baada ya leo tena kuifungia Simba SC mabao mawili katika ushindi wa 3-0 iliyoupata dhidi ya Mwadui FC kutoka Shinyanga.
Okwi amefunga mabao hayo kwa ustadi wa hali ya juu katika dakika ya 7, na 67 kabla ya nahodha wa Simba katika mchezo wa leo, John Bocco kupiga bao la tatu dakika ya 72.
Magoli hayo ya Okwi yanamfanya awe kinara wa kupachika magoli katika ligi kwa kufikisha magoli sita ndani ya mechi mbili alizocheza, huku John Bocco akifungua rasmi akaunti ya mabao likiwa ni bao lake la kwanza akiwa ndani ya uzi mwekundu wa mitaa ya Msimbazi.
Kikosi cha Simba kwenye mchezo huo kilikuwa na mabadiliko makubwa huku wachezaji ambao huwa hawapati nafasi mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza, wakijumuishwa kwenye kikosi.
Wachezaji waliopata nafasi leo ni pamoja na Juuko Murshid, Mohamed Hussein, Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto na Laudit Mavugo.
Nao Mbeya City waliopoteza mchezo uliopita dhidi ya Ndanda wameibuka na ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Mji Njombe kwa goli la mchezaji Elyud Ambokile dakika ya 34 ya mchezo.



0 comments :
Post a Comment