Mke wa Rais na Mwenyekiti wa
WAMA, Mama Salma Kikwete akipokea TUZO maalum ya “ CWL International
Women of Excellency Award for Leadership” kutoka kwa Profesa Joseph
Adaikalam, Mwanzilishi na Mtendaji Mkuu wa Chuo Kukuu cha Binary
kilichoko nchini Malaysia kwa kutambua na kuthamini mchango wake katika
maendeleo ya wanawake nchini Tanzania na Afrika tarehe 24.7.2015.
Aliyesimama (kushoto) ni Balozi wa Tanzania nchini Malaysia Dkt. Aziz
Mlima, akifuatiwa na Profesa Bulochana Nair na Kulia ni Profesa Datin
Rohini Devi wa Chuo Kikuu cha Binary.
PICHA NA JOHN LUKUWI.
……………………………………………………………………………………………….
Na Anna Nkinda – Kuala Lumpur, Malaysia
Mke wa Rais Mhe. Mama Salma
Kikwete ametunukiwa tuzo ya kimataifa ya mwaka 2015 ya Kiongozi bora
Mwanamke (International Woman of Excellence Award for Leadership) na
kituo cha Uongozi cha wanawake cha chuo kikuu cha Binary cha nchini
Malaysia kutokana na mchango wake mkubwa katika uhamasishaji wa
maendeleo ya wanawake watanzania.
Tuzo hiyo imetolewa leo na
Mwanzilishi na Mwenyekiti Mtendaji wa chuo hicho Prof. Joseph Adaikalam
katika ukumbi wa mikutano uliopo chuo kikuu cha Binary kilichopo Kuala
Lumpur nchini Malaysia.
Akiongea mara baada ya
kukabidhiwa tuzo hiyo Mhe. Mama Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi
ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alikishukuru kituo hicho na kusema
amefarijika kwa kuona jinsi kinavyothamini maendeleo ya Wanawake wa
Afrika na Dunia kwa ujumla. Kwa kupitia tuzo hiyo wameonesha jinsi
wanavyotambua na kuthamini juhudi zinazofanywa na wanawake.
Mhe. Mama Kikwete alisema “Tuzo
hii siyo yangu pake yangu bali ni ya ushindi wa wanawake wote wa
Tanzania, Afrika na maeneo mengine ambao wanafanya jitihada kubwa ya
kukabiliana na vikwazo kadhaa vinavyowazuia kupiga hatua kubwa ya
maendeleo. Mafanikio yanayoonekana yanapatikana ingawaje safari bado ni
ndefu na yenye changamoto nyingi”.
Nilipoanza majukumu yangu kama
Mke wa Rais wa nchi yetu, nilitambua umuhimu wa kuwa na chombo
kitakachoniwezesha kuhamasisha jamii na rasilimali ili niweze kutoa
mchango wangu kwa ajili ya maendeleo ya jamii yetu. Hivyo nilianzisha
Taasisi ya WAMA ikiwa na Dira ya kuiona Tanzania ambayo wanawake
wanawezeshwa na kuishi maisha bora”.
Aliendelea kufafanua kwamba tangu
awali alitambua ili kumkomboa mwanamke ni muhimu kuzingatia mazingira
na mahitaji yake yote kwa pamoja. Alitambua kwa kumpatia mtoto wa kike
elimu, kutamuepusha na ndoa za utotoni, ujauzito katika umri mdogo,
kutapunguza matukio ya vifo vinavyotokana na uzazi na vifo vya watoto
wachanga.
Mwenyekiti huyo wa WAMA
alimalizia kwa kusema kuwa mwanamke aliyeelimika anatambua na kuweza
kutumia fursa za kiuchumi na kujiendeleza yeye mwenyewe na jamii
inayomzunguka.
Akisoma wasifu wa Mhe. Mama
Kikwete Prof. Sulochana Nair ambaye ni Makamu na Mtendaji Mkuu wa Chuo
hicho alisema tuzo hiyo ni ya juu na kwa mara ya kwanza imetolewa kwa
mke wa Rais hii ni kutokana na kazi anazozifanya za kuwasaidia wanawake,
watoto na watanzania kwa ujumla.
Prof. Sulochana alisema Mama
Kikwete kupitia Taasisi ya Wama ametoa fursa za elimu ya sekondari kwa
watoto wa kike ambao ni yatima na wengine wanaotoka familia masikini
hadi sasa zaidi ya watoto 800 wamenufaika, kufanya uraghibishi dhidi ya
ndoa za utotoni, mimba katika umri mdogo.
Kupiga vita maambukizi ya VVU kwa
vijana na kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ,kufanya uraghibishi ili
kuishirikisha jamii katika kutoa chanjo, upimaji na matibabu ya saratani
za shingo ya kizazi na matiti, kutoa mafunzo na uratibu wa kuwawezesha
wanawake kiuchumi.
Tuzo ya kimataifa ya Kiongozi
bora Mwanamke (International Woman of Excellence Award for
Leadership)inayotolewa na kituo hicho pale wanapoona na kutambua mchango
wa mwanamke aliyejitokeza kwa juhudi zake za kusaidia na kuhamasisha
maendeleo ya wasichana na wanawake Duniani.
0 comments :
Post a Comment