Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amewaonya askari wa Kikosi cha Usalama barabarani kutogeuza tochi kuwa chanzo cha kudai rushwa.
Pia, amewataka kutowanyanyasa madereva ambao wanazingatia sheria za usalama barabarani.
Kwa upande wa madereva amewataka kuwaona askari hao kuwa ni walinzi wao.
Amesema hayo leo, Jumatatu katika uzinduzi wa maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani uliofanyika kitaifa mkoani Kilimanjaro katika viwanja vya Mashujaa mjini Moshi.
Samia amesema takriban asilimia 76 ya ajali za barabarani husababishwa na makosa ya kibinadamu kutokana na utumiaji wa simu wakati wa kuendesha gari, uchovu wa madereva na ulevi.
Amesema sababu nyingine zinazochangia ajali za barabarani ni miundombinu mibovu ya barabara inayochangia kwa asilimia nane na ubovu wa magari unaochangia kwa asilimia 16.
Makamu wa Rais amesema idadi kubwa ya ajali hizo zinasababishwa na uzembe wa waendesha bodaboda ambao unaweza kuepukika.
Samia amesema Taifa limeendelea kupoteza nguvu kazi, watu kupata ulemavu wa maisha na wengine kubaki wajane.
“Mwaka huu kuanzia Januari hadi Septemba kumekuwa na ajali za pikipiki 42,721 zilizoua watu 1,613 na kusababisha majeruhi 1,597,” amesema.
Amesema Mkoa wa Kilimanjaro umeripotiwa kuwa na ajali 84 za bodaboda zilizosababisha vifo 61 na majeruhi 21.
Samia ameeleza kusikitishwa kwa Tanzania kutajwa katika ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kuwa ni nchi inayoongoza kwa ajali ikiwa na asilimia 33.
Ameliagiza Baraza la Taifa la Usalama Barabarani kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani na wadau kuzingatia na kuelekeza nguvu kwenye kudhibiti makosa makubwa matano hatarishi.
Kwa upande wa abiria, amewataka kutosita kutoa taarifa pale sheria inapovunjwa na madereva.