Jeshi la Polisi limewatahadharisha viongozi wa makundi ya WhatsApp kuwa makini na kutoa taarifa muhimu pindi uhalifu unapofanyika kupitia makundi yao.
Tamko hili katika kikao cha pamoja kati ya polisi na wadau wa mawasiliano nchini, waliokuwa wakiangalia na kujadili masuala mbalimbali yanayohusu matumizi ya mitandaoni kufuatia kukithiri kwa makosa ya kimtandao huku makundi ya WhatsApp yakionekana kuwa kichocheo kikubwa zaidi.
Kwa mujibu wa mwakilishi wa jeshi la polisi nchini, viongozi hao wa makundi wametakiwa kutowavumilia watakaotenda makosa hayo na hivyo kuhimizwa kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi.
“Usikubali kuharibiwa wakati umeanzisha kundi kwa nia nyingine halafu mtu au watu wanaweka mambo yasiyofaa, toa taarifa hatua zichukuliwe kinyume na hapo hata wewe utahusika,” .
Mwakilishi wa Polisi amesema kwa kiasi kikubwa makundi ya WhatsApp yamekuwa yakitumika kusambaza taarifa za uongo na uchochezi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa TCRA, Mhandisi James Kilaba amesema mamlaka hiyo inaendelea kuchukua hatua madhubuti katika kuimarisha ulinzi wa mawasiliano mtandaoni.
Amesema simu za mkononi kwa sasa zimekuwa kama silaha hivyo matumizi yake yanapaswa kuangaliwa kwa umakini zaidi.