18DEC 2017 NA MWANDISHI WETUHABARI
Nipashe
Polisi wawili watiwa mbaroni Takukuru
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imesema inachunguza watendaji wanne wa serikali wakiwamo askari polisi wawili kwa tuhuma za rushwa.
Wanaochunguzwa na taasisi hiyo nyeti ni wanasheria wawili wa Baraza la Uhifadhi wa Mazingira (Nemc), Bernard Kongole na Lucy Lwigisha na askari wawili wa Kituo cha Polisi Mbweni, Kinondoni jijini Dar es Salaam, wote wakituhumiwa kwa rushwa ya Sh. milioni moja.
Wanne hao wanadaiwa kuomba rushwa hiyo kwa mkalimani ambaye ni raia wa China ambaye anafanya kazi kwenye kiwanda cha uzalishaji mifuko ya sandarusi cha Yong Long Plastic Co. Limited kilichopo Tegeta IPTL jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kinondoni, Thed Mjangira, alithibitisha taasisi hiyo kuwashikilia watu hao huku akibainisha kuwa upelelezi kuhusu suala hilo unaendelea.
"Ni kweli tuliwaita kwa ajili ya kufanya nao mahojiano baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema kwamba watu hao waliomba na kushawishi wapewe rushwa,” Mjangira alisema.
“Na naomba tu kwa sasa niseme hivyo kwa sababu upelelezi hauwezi kukamilika siku moja, tusubiri mpaka utakapokamilika kwa sababu bado tunaendelea kulifanyia uchunguzi zaidi.” Inadaiwa kuwa Novemba 17, mwaka huu, Kongole na Lugwisha walikwenda Tegeta kwenye kiwanda hicho kwa lengo la kukagua kibali cha uendeshaji wa shughuli hizo na walimkuta mkalimani binafsi wa Wachina wanaokimiliki na ndiye alikuwa akiwaongoza katika mazungumzo yao.
Inadaiwa kuwa mkalimani huyo baada ya kumaliza kuwaongoza katika mazungumzo hayo, aliondoka huku akiacha gari lake kiwandani hapo.
Hata hivyo, inadaiwa kwamba mazungumzo baina ya Wachina na wanasheria hao wa Nemc hayakufikia mwafaka kama walivyotarajia.
Inadaiwa kuwa licha ya mazungumzo hayo kutokamilika, mkalimali huyo aliamua kuondoka na kuwaacha ili kuwahi majukumu yake mengine kwa kuwa aliona kama anachelewa na hivyo kukodi pikipiki na kuacha gari lake.Inadaiwa kuwa kitendo hicho hakikumfurahisha Kongole ambaye aliwaamuru polisi kulichukua gari hilo na kuondoka nalo hadi Kituo cha Polisi.
Inadaiwa kuwa baada ya kufika kituoni, Kongole aliandika maelezo ya kuwashikilia Wachina hao kwa madai ya kuendesha shughuli zao bila kibali cha Nemc na kutakiwa kuwapeleka Kituo cha Polisi Mbweni.
Siku iliyofuata, inadaiwa kuwa mkalimani huyo alifika katika Kituo cha Polisi Mbweni kufuatilia gari lake, lakini aliambiwa kuwa anatakiwa kutoa Sh. milioni 1.3.
Inadaiwa kuwa mkalimani huyo aliambiwa Sh. milioni moja zitatumika kufuta kesi na Sh. 300,000 ni kwa ajili ya fedha za maegesho ya kulaza gari kwenye Kituo cha Polisi Tegeta ambako gari hilo lilikuwa linahifadhiwa.
Kutokana na hali hiyo, inadaiwa kuwa mkalimani huyo alitoa Sh. 300,000 kulipia maegesho ya gari, lakini alishindwa kutoa Sh. milioni moja kwa madai kuwa hakuwa na fedha.
Mbali na wanne hao, Mjangira alibainisha kuwa kuna watu wengine wanaohojiwa na Takukuru kuhusu tukio hilo wakiwamo askari polisi wengine wa Kituo cha Polisi Mbweni, Mkuu wa Kituo cha Polisi Mbweni, Pastory Mathias na Ofisa Upelelezi wa kituo hicho aliyemtaja kwa jina moja la Rugemalira.
Nipashe ilimtafuta kwa simu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, ili kuzungumzia tukio hilo, lakini alisema hakuwa na taarifa nalo na kuahidi kulifuatilia, hata hivyo.
“Sina taarifa kama kuna polisi wanahojiwa na Takukuru kwa sababu ya kuomba au kushawishi rushwa, naomba nilifuatilie kwanza,” alisema Mambosasa.
0 comments :
Post a Comment