Wabunge Wa Tanzania Na Burundi Wagoma Kumtambua Spika Wa EALA


 Dk Martin Ngonga 
Siku moja baada ya Bunge la Afrika Mashariki (Eala) kumchagua Spika mpya atakayekiongoza chombo hicho kwa kipindi cha miaka mitano, wabunge wa Tanzania na Burundi wametangaza kutomtambua spika huyo kwa madai ya kanuni za uchaguzi kutozingatiwa.

Kufuatia hali hiyo, wabunge kutoka Tanzania wamesema hawatashiriki vikao vya Bunge hilo.
 
Kwa nyakati tofauti wabunge hao wamezungumza na wanahabari Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na kueleza mtazamao wao kuhusu ushindi wa Spika huyo, Dk Martin Ngonga kutoka Rwanda.


Mwenyekiti wa wabunge wa Tanzania, Dk Abdullah Makame amesema uendeshaji wa shughuli za jumuiya hiyo unapaswa kufanywa kwa maridhiano tofauti na kilichotokea juzi.



Amebainisha kuwa kutokana na hali ilivyo hawatahudhuria vikao vya Bunge hilo kwasababu hakukua na maridhiano ya namna uchaguzi unapaswa kufanyika kwa kuzingatia akidi ya wajumbe.


“Wakati uchaguzi unafanyika wabunge wa Tanzania na Burundi waligoma,” amesisitiza.
 
Amesema licha ya nchi ya Kenya kuwa ni mwasisi wa jumuiya imechelewesha mara mbili kuanza kwa bunge la Eala, mara ya kwanza ikiwa ni mwaka 2007 na mwaka huu tena imetokea lakini walisubiriwa katika utaratibu wa maridhiano ili kulinda umoja huo.


"Ikitokea kutoelewana kwenye jambo lolote namna ya kulimaliza ni maridhiano. Kama wawili wakisema ndio na mmoja akasema hapana inabidi hilo jambo lisifanyike,” amesema.


Amesisitiza, “mtakumbuka bunge hili limechelewa kuanza kwa kipindi cha miezi sita kwa ajili ya kuisubiri nchi ya Kenya ifanye uchaguzi.”


Uchaguzi huo uligubikwa na vuta nikuvute kutokana na madai ya baadhi ya wabunge kuwa ulifanyika licha ya kutotimia kwa akidi baada ya wabunge tisa wa Burundi na saba wa Tanzania kutokuwepo kwa sababu ambazo hazikujulikana.


Makame amesema ili kujenga jumuiya imara ni lazima kila nchi iheshimiwe inapotoa mawazo yao badala ya kupuuzwa, kwamba inaweza kusababisha kuwa na jumuiya dhaifu ambayo haiwatumikii wananchi wake ipasavyo.


Akizungumzia sababu ya mbunge kutoka Tanzania, Adam Kimbisa kuwania uspika wakati zamu yao ilishapita, amesema mara baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) walipewa barua zinazowataka wabunge wenye nia ya kugombea wafanye hivyo isipokua nchi ya Uganda ambayo Spika aliyemaliza muda ametokea huko.


Naye Dk Ngware Maghembe amesema ili kupata makamishna wawili, kila nchi ni lazima kuwepo na akidi ya wabunge wote, iwapo haitakuwepo Bunge halitaweza kuendelea na majukumu yake ya kuunda kamati.


Hata hivyo, Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa bunge hilo, Bob Odiko akitolea ufafanuzi hoja ya akidi alisema utaratibu huo unafanya kazi wakati Bunge likiwa limekaa chini ya uongozi wa Spika na sio Katibu wa Bunge.


Wabunge wa Burundi ambao walifanya mkutano na waandishi wa habari kumlalamikia Katibu wa Bunge, Kenneth Madete kutokujibu barua yao waliyotaka ofisi yake itoe tafsiri ya nafasi ya Spika kuwa ni mzunguko kwa nchi wanachama.


Kutokana na barua hiyo kutojibiwa waliendelea kugomea kikao cha jana cha kuwachagua makamishna sanjari na wabunge wa Tanzania.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment