Hiki Hapa Chanzo Cha Ajali Ya Aliegongwa Na Ndege Mwanza


KAMANDA wa Polisi wa Viwanja vya Ndege nchini, Matanga Mbushi, ameweka bayana chanzo cha mwanamke aliyegongwa na ndege ya Fastjet jijini Mwanza na kufariki dunia kuwa alikuwa na matatizo ya akili.

Akizungumza na Nipashe jana, Kamanda Mbushi alisema hadi sasa wameshindwa kubaini jina la mwanamke huyo ambaye alifariki dunia papo hapo baada ya kugongwa na ndege.

Ajali hiyo ilitokea katikati ya wiki iliyopita usiku kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwanza, ulioko wilayani Ilemela.

Ndege hiyo ilimgonga mwanamke huyo akiwa anavuka kwenye njia ya kurukia ndege  wakati ndege hiyo yenye namba za usajili 58S-EJE190 ikiwa kwenye mwelekeo wa kuruka.

Alipoulizwa jana kama mwanamke huyo amefahamika na hatua gani zinachukuliwa ili tukio hilo lisitokee tena, Kamanda Mbushi alisema wanaopaswa kuzungumzia hilo ni Mamlaka ya Usalama wa Anga (TCAA).

“Yule mwanamke bado hatujapata jina lake, lakini inavyoonekana kuwa alikuwa na matatizo ya akili,” alisema.

Akizungumza na gazeti hili Ijumaa iliyopita, Kamanda huyo alisema wakati ndege hiyo ikiwa kwenye mwelekeo wa kuruka, mwanamke huyo alikuwa anakatiza kwenye njia ya ndege ndipo alipogongwa na kufa papo hapo.

“Ndege hii ilikuwa kwenye mruko wa futi 148 tokea pointi 12 kuelekea pointi 30 ikiwa na abiria 89 waliokuwa wakitoka Mwanza kwenda Dar es Salaam,” alisema.

Alisema pamoja na ajali hiyo, ndege hiyo iliruka na kusafiri salama hadi Dar es Salaam.

Matukio ya ndege kugonga mtu ni nadra kutokea duniani kwa mujibu wa utafiti wa Nipashe, lakini ajali inayokaribiana na ya Mwanza ni ile iliyotokea katika jimbo la California, Marekani Aprili 3, 2016.

Katika ajali hiyo, mtu mmoja alifariki baada ya ndege ndogo kuangukia gari lililokuwa barabarani.

Mashuhuda, kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), walisema ndege hiyo ilionekana kama ilikuwa na matatizo ya injini na ikalazimika kutua kwa dharura kwenye barabara ya magari.

Rubani wa ndege hiyo aliyetajwa kuwa Dennis Hogge, alishindwa kuidhibiti na ikateleza na kugonga gari lililokuwa na watu wanne lililokuwa limeegeshwa kando ya barabara hiyo, ili dereva azungumze kwa simu.

Mtu mmoja alifariki dunia hapo hapo huku wengine watatu wakipelekwa hospitalini. Mtu aliyefariki dunia, Antoinette Isbelle (38), kutoka mji wa San Diego alikuwa ameketi nyuma katika gari hilo lililogongwa.

Katika hali ya kushangaza, haikuwa mara ya kwanza kwa ndege hiyo kutua kwenye barabara hiyo ya San Diego.

Mwaka 2000 mmiliki wa kwanza wa ndege hiyo alipatwa na hitilafu ya kimitambo na akalazimika kutua ndege aina ya Lancair 1V, kwenye barabara hiyo hiyo, BBC iliripoti.

Hata hivyo, tukio hilo halikusababisha maafa wala uharibifu wa ndege hiyo.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment