Jeshi la Polisi mkoani hapa lilimshikilia na kumuachia kwa dhamana Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa kwa tuhuma za kuratibu matukio mawili ya kihalifu likiwamo la kuchoma nyumba aliyokuwa akiishi Katibu wa Jumuiya ya Vijana wa CCM Iringa Mjini, Alfonce Muyinga.
Kamanda wa polisi mkoani hapa, Julisu Mjengi amesema mbunge huyo alikuwa akitafutwa kwa muda akituhumiwa kuratibu utekelezwaji wa matukio mawili ya kihalifu likiwamo la Januari 17 la kuchomwa kwa nyumba aliyokuwa akiishi Muyinga.
Mjengi alitaja tukio la pili kuwa ni lile la Januari 15 la kubomolewa kwa nyumba ya aliyekuwa Diwani wa Kata ya Mwangata Chadema, Anjelus Mbogo aliyejizulu nafasi yake na kuhamia CCM.
"Mchungaji Msigwa tulikuwa tukimtafuta kutokana na kuhusika kwake katika kuratibu matukio mawili ya kihalifu, lile la Januari 15 la kubomoa nyumba ya aliyekuwa diwani aliyehama Chadema na kujiunga na CCM pamoja na tukio la kuchoma nyumba aliyokuwa akiishi Katibu wa Jumuiya ya Vijana wa CCM Alfonce," amesema Mjengi na kuongeza;
"Na jana (Jumatatu) amejisalimisha mwenyewe hivyo tumemhoji hadi majira ya saa tatu usiku tulipomuachia kwa dhamana, taratibu nyingine zinaendelea na tutawajulisha pindi tukapozikamilisha," amesema
Msigwa amekuwa mtuhumiwa wa nne kukamatwa akihusisha na matukio hayo baada ya wiki iliyopita jeshi hilo kueleza kuwa linawashikiliwa watuhumiwa watatu kwa mahojiano kutokana na kuhusika na tukio la kuchoma nyumba ya aliyokuwa akiishi Katibu wa UVCCM.
0 comments :
Post a Comment